• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Kane na Saka watawazwa Wachezaji Bora wa Mwaka 2021 katika EPL kutoka jijini London

Kane na Saka watawazwa Wachezaji Bora wa Mwaka 2021 katika EPL kutoka jijini London

Na MASHIRIKA

MWANASOKA Harry Kane wa Tottenham Hotspur ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutoka jijini London baada ya kuwapiku wanasoka Son Heung-min, Mason Mount na Declan Rice.

Kiungo mvamizi wa Arsenal, Bukayo Saka ndiye aliyetawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka kwenye tuzo hizo.

Kane, 27, anajivunia kufungia Spurs jumla ya mabao 31 na kuchangia mengine 16 kutokana na jumla ya michuano 44 kufikia sasa msimu huu.

Ufanisi huo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Kane ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza kutia kibindoni taji hilo.

Mbali na Son ambaye hushirikiana na Kane katika safu ya mbele ya Spurs, wanasoka wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Mount wa Chelsea na masogora wawili wa West Ham United – Rice na Tomas Soucek.

Japo Rice na Soucek waliambulia pakavu, mkufunzi wao David Moyes alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka huku mlinda-lango wao Lukasz Fabianski akitwaa taji la Kipa Bora wa Mwaka.

West Ham ni miongoni mwa vikosi vinavyofukuzia nafasi ya kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora msimu huu na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao wa 2021-22.

Saka, 19, anajivunia kufungia Arsenal jumla ya mabao tisa katika EPL kufikia sasa msimu huu licha ya waajiri wake kusuasua pakubwa kwenye kampeni za kivumbi hicho.

Saka ambaye ni raia wa Uingereza aliwapiku Rice, Mount, Reece James wa Chelsea na Emile Smith Rowe ambaye ni mwenzake kambini mwa Arsenal kwenye tuzo hizo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Afueni kwa West Ham Utd kadi nyekundu ambayo beki Balbuena...

Safari za Madaraka Express zaleta matumaini Pwani baada ya...