Wawili wafariki, mmoja ajeruhiwa kwenye shambulio la al-Shabaab Lamu

Na KALUME KAZUNGU

WATU wawili waliuawa huku mmoja akijeruhiwa Jumatatu pale gari walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga kilipuzi kinachoshukiwa kutegwa ardhini na wapiganaji wa al-Shabaab, Kaunti ya Lamu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amesema shambulio hilo lilitekelezwa saa tatu na nusu asubuhi.

Kulingana na Bw Macharia, gari lililokuwa limebeba mafundi watatu wa ujenzi lilikanyaga kilipuzi hicho eneo la Border Point 27 lililoko kilomita chache kutoka kijiji cha Ishakani, kaunti-ndogo ya Lamu Mashariki.

Tukio hilo lilisababisha gari kuharibiwa vibaya na kuwaacha wawili wakiwa wameaga dunia naye mmoja akiachwa na majeraha mabaya.

“Gari la maafisa wa ujenzi kutoka Ishakani kuelekea eneo la Border Point 27 lililoko mpakani mwa Lamu na Somalia lilikanyaga kilipuzi cha kutegwa ardhini na kuharibiwa vibaya. Wawili walifariki papo hapo naye mmoja amejeruhiwa vibaya,” akasema Bw Macharia.

Amesema maafisa wa usalama, ikiwemo polisi na wanajeshi wa Kenya (KDF) walifika haraka kwenye eneo la shambulio.

“Kwa sasa operesheni ya kuwatafuta waliotekeleza shambulio hilo inaendelea. Watu wasiwe na hofu. Waendelee kushirikiana na walinda usalama wetu na kupiga ripoti iwapo watashuhudia tukio au mtu yeyote wanayemshuku kuwa kero kwa usalama,” akasema Bw Macharia.

Shambulio hilo linajiri mwezi mmoja baada ya mtu mmoja kufariki pale lori walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga kilipuzi kinachoshukiwa kuzikwa ardhini na wapiganaji wa al-Shabaab kilomita chache kutoka mjini Kiunga.

Lori hilo lilikuwa likisafirisha maji kutoka eneo la Kiunga kuelekea Kambi ya Usalama iliyoko mpakani mwa Kenya na Somalia ili kutumika kwa ujenzi unaoendelea wa ukuta wa usalama kwenye mpaka huo.

Aliyefariki alikuwa utingo wa lori husika ilhali dereva wake aliponea bila majeraha yoyote.

Mnamo Januari 2016, maafisa watano wa polisi waliuawa pale gari walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga kilipuzi cha kutegwa ardhini kilomita chache kutoka Milimani, kwenye barabara kuu ya Hindi kuelekea Kiunga.

Shambulio hilo pia lilitekelezwa na wapiganaji wa al-Shabaab wakati gari hilo likisafirisha maafisa hao kuelekea kambi ya ujenzi wa ukuta wa kutenganisha Kenya na Somalia katika eneo la mpakani.

Mradi wa kujenga ukuta huo wa urefu wa kilomita 700 ulizinduliwa na serikali ya kitaifa mnamo 2015, dhamira kuu ikiwa ni kudhibiti kuvuka ovyo kwa al-Shabaab kutoka Somalia kuingia Kenya kutekeleza mashambulio.

Habari zinazohusiana na hii