• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
TAHARIRI: Uhuru wa habari ulindwe kikamilifu

TAHARIRI: Uhuru wa habari ulindwe kikamilifu

KITENGO CHA UHARIRI

WANAHABARI humu nchini jana Jumatatu walijiunga na wenzao ulimwenguni kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari.

Siku hii inayoadhimishwa kila mwaka huwa ni muhimu kwa wadau wa sekta ya habari kufanya utathmini kuhusu hali ilivyo, changamoto zilizopo na suluhisho zinazoweza kusaidia kuboresha kazi ya uanahabari.

Katika maadhimisho ya jana, sawa na nyingine za miaka iliyopita, masuala yaliyoibuka sana ni kuhusu ukandamizaji wa wanahabari wanapokuwa kazini. Hili ni jambo ambalo limekuwa donda sugu mno sio Kenya pekee bali ulimwenguni kote.

Wanahabari wengi huishi kwa hofu, sio kwa kuwa wametenda uhalifu wowote bali kwa kuwa wamefanya kazi yao vyema kuanika maovu yaliyo katika jamii.

Vitisho vya mara kwa mara na hata kupigwa na kuuawa kwa wanahabari ni mambo ambayo yanasababisha dhiki tele katika sekta hii muhimu.

Ijapokuwa Kenya imepiga hatua kubwa katika kukuza na kulinda uhuru wa wanahabari wanapofanya kazi zao ikilinganishwa na nchi nyingine za barani Afrika, bado kuna pengo linalofaa kuzibwa.

Suala la wanahabari kutishiwa maisha yao wanapofanya kazi linafaa lichukuliwe kwa uzito zaidi ya jinsi ilivyo kwa sasa. Vile vile, maafisa wanaohusika katika kushambulia wanahabari peupe pia wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria wala si kulindwa kamwe.

Kando na haya, vitendo vingine ambavyo hutekelezwa kusudi kuathiri kazi ya uanahabari pia vinafaa vikomeshwe. Hivi ni kama vile upitishaji sheria za kukandamiza kuhusu wa wanahabari, serikali kunyima wanahabari ripoti muhimu za kitaifa ili kuficha maovu ya utawala ulio mamlakani, na katika siku za hivi majuzi, watumizi wa mitandao ya kijamii kufadhiliwa ili kuharibia wanahabari na vyombo vya habari sifa bila sababu.

Wananchi wana haki ya kusambaziwa habari muhimu zinazoaminika, na hilo halitafanikishwa kikamilifu iwapo tutaendelea kushuhudia hali ambapo wanahabari hawapewi nafasi ya kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ni kupitia kwa habari za kuaminika ambapo raia wanaweza kuchukua hatua zinazofaa ili wachangie kikamilifu katika kuendesha gurudumu la maendeleo ya taifa.

Haki ya umma kupokea habari imelindwa kikatiba na hivyo basi haifai kamwe haki hiyo ivurugwe kwa njia yoyote ile.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Wanafunzi 700 Lugari hawana madarasa shule...

ODONGO: Malumbano ODM ni ishara ya juhudi za kumrithi Odinga