• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
ODONGO: Malumbano ODM ni ishara ya juhudi za kumrithi Odinga

ODONGO: Malumbano ODM ni ishara ya juhudi za kumrithi Odinga

Na CECIL ODONGO

UBABE kati ya Seneta wa Siaya James Orengo na baadhi ya wabunge waaminifu kwa Kinara wa ODM Raila Odinga, unaonyesha wazi kwamba mikakati ya kichinichini inaendelea kurithi ufalme wa kisiasa katika eneo la Luo Nyanza kutoka kwa Waziri huyo Mkuu wa zamani.

Japo kiini cha uhasama wao wiki jana bungeni kilikuwa iwapo mswada wa Jopokazi la Maridhiano (BBI), unafaa kufanyiwa marekebisho au la, cheche kali kati yao zilionyesha wazi kuwa suala kuu ni kudhibiti siasa za eneo hilo.

Bw Odinga amekuwa mfalme wa kisiasa za Waluo kwa karibu miaka 30 na huenda ushawishi wake ukapungua iwapo hatakuwa debeni 2022.

Wabunge Opiyo Wandai (Ugunja), Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Kiranja wa wachache Junet Mohamed, ni viongozi waliokuwa katika mstari wa mbele kumkemea Bw Orengo na mbunge wa Rarieda Otiende Amolo ambao sasa wanachukuliwa kuwa wasaliti.

Ingawa Mabw Orengo na Odinga wamewahi kuwa na uhasama wa kisiasa kati yao miaka ya nyuma, wabunge chipukizi hawafai kutumia ukuruba wao na Bw Odinga kumkosea heshima Seneta huyo wa Siaya ambaye amesimama na Bw Odinga nyakati ngumu zaidi kisiasa.

Kuhusu BBI, kauli ya Bw Orengo ni sawa kwa sababu mswada huo una mapungufu kadhaa na maeneobunge mapya hayajagawanywa kwa usawa huku eneo la Luo Nyanza likiwa kati ya maeneo yaliyobaguliwa.

Kaunti hizo nne zenye idadi kubwa ya watu zitaongezewa maeneobunge manne pekee huku Kaunti ya Migori ikikosa kupata eneobunge jipya. Kisumu itakuwa na maeneobunge mapya mawili, huku Homa Bay na Siaya zikipata eneobunge moja kila moja.

Hili ni kati ya masuala ambayo Seneta huyo alilalamikia kabla ya kukemewa na Mabw Mbadi, Junet na Wandayi ambao ni vibaraka na wanafuata mambo mradi tu Bw Odinga aseme na aridhike.

Baada ya kurudi kambini mwa Bw Odinga na kushinda kiti chake cha Ugenya 2007, Bw Orengo amekuwa wa msaada mkubwa kwa Waziri huyo Mkuu wa zamani ikilinganishwa na wakati walitofautiana kisiasa.

Alikuwa katika kamati iliyoafikiana kuhusu kubuniwa kwa serikali ya muungano 2008, akawa kati ya wanasheria walioandika Katiba mpya 2010 na pamoja na Bw Amollo, walikuwa kati ya wanasheria waliowakilisha NASA katika kesi ya kupinga matokeo ya Urais 2017.

Sawa tu na Bw Odinga, Seneta huyo ana historia ya uanaharakati na utetezi, akiwa kati ya waliopigania mfumo wa vyama vingi miaka ya 80 na mapema 90. Bw Orengo alikuwa mwandani wa babake Raila, marehemu Oginga Odinga katika chama cha Ford Kenya hadi kifo cha kigogo huyo wa siasa za upinzani 1994.

Je, Mabw Mbadi, Wandayi na Junet wamemfaa Bw Odinga kivipi kiasi kwamba wanamrejelea Bw Orengo kuwa msaliti ilhali anasema

ukweli kuhusu mapungufu ya BBI?

Wabunge hawa wana safari ndefu ya kurithi ufalme wa Bw Odinga kisiasa na vyeo wanavyoshikilia ndani ya ODM havifai kuwahadaa kuwa wao ni maarufu miongoni mwa wapigakura.

Ingawa wanafikiria kuwa BBI ndiyo tiketi ya kuhakikisha Bw Odinga anaingia ikulu, siasa hubadilika na huenda mswada huo ukakosa kutimiza malengo yao.

Aidha, Bw Odinga hakupewa ubabe wa siasa za Waluo ila aliupigania licha ya upinzani mkali kutoka kwa Bw Orengo na Gavana wa sasa wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o.

Kwa hivyo, anayesaka wadhifa huo ajiuze kwa wananchi badala ya kuwalenga wengine na kuwaita wasaliti.

Wananchi wameerevuka na kumfuata Bw Odinga kama kipofu si tiketi ya umaarufu wa mwanasiasa yeyote katika siasa za Luo Nyanza.

You can share this post!

TAHARIRI: Uhuru wa habari ulindwe kikamilifu

WANGARI: Maslahi ya Wakenya wanaougua Ukimwi yasipuuzwe