• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Manchester City wazamisha chombo cha PSG na kuingia fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza katika historia

Manchester City wazamisha chombo cha PSG na kuingia fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza katika historia

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walitinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kuwapepeta Paris Saint-Germain (PSG) 2-0 katika mkondo wa pili wa nusu-fainali ugani Etihad mnamo Jumanne na hatimaye kuwadengua kwa jumla ya mabao 4-1.

Riyad Mahrez ambaye ni raia wa Algeria, aliwafungia Man-City mabao yote mawili katika mchuano huo wa marudiano katika dakika za 11 na 63 mtawalia. Magoli hayo ya Mahrez yalichangiwa na kipa Ederson Moraes na kiungo chipukizi Phil Foden.

PSG waliokosa huduma za fowadi matata Kylian Mbappe katika mechi hiyo kutokana na jeraha, walipatwa na pigo jingine katika dakika ya 69 baada ya mshambuliaji Angel Di Maria kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo kiungo Fernandinho.

Ilikuwa mara ya pili mfululizo kwa PSG kukamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Idrissa Gueye kuonyeshwa pia kadi nyekundu katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliochezewa ugani Parc des Princes, Ufaransa mnamo Aprili 28, 2021.

Japo PSG walipewa penalti kwa madai kwamba Oleksandr Zinchenko alikuwa ameunawa mpira, maamuzi hayo yalibatilishwa na teknolojia ya VAR. Huku Neymar akikabwa vilivyo na mabeki wa Man-City, kikosi cha kocha Mauricio Pochettino kilionekana kuzidiwa maarifa katika kila idara.

Man-City kwa sasa watakutana ama na Chelsea au Real Madrid kwenye fainali ya UEFA itakayochezewa jijini Istanbul, Uturuki mnamo Mei 29, 2021.

Ufanisi huo unaweka hai matumaini ya kocha Pep Guardiola na Man-City kutia kapuni jumla ya mataji matatu msimu huu baada ya kujizolea ubingwa wa Carabao Cup.

Aidha, miamba hao wako pua na mdomo kujinyanyulia ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na huenda wakatawazwa mabingwa mnamo Mei 8 iwapo watasajili angalau sare ya aina yoyote dhidi ya Chelsea ugani Etihad.

PSG waliozidiwa ujanja na Bayern Munich kwenye fainali ya UEFA mnamo 2019-20, sasa wanaelekeza makini yao kwenye kipute cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ambapo pia wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwapita Lille kileleni mwa jedwali.

Isitoshe, miamba hao wa soka ya Ufaransa wameratibiwa kuvaana na Montpellier kwenye fainali ya French Cup mnamo Mei 12, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Huzuni yatanda aliyeuawa kwenye shambulio la al-Shabaab...

Sergio Ramos roho juu kuongoza Real Madrid kuangusha...