• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Kutokuwepo kwa Mbappe si kisingizio cha PSG kupigwa na Manchester City – Pochettino

Kutokuwepo kwa Mbappe si kisingizio cha PSG kupigwa na Manchester City – Pochettino

Na MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino amefutilia mbali madai kwamba kutokuwepo kwa fowadi Kylian Mbappe katika kikosi chake cha Paris Saint-Germain (PSG) ni sababu kuu ya kupigwa kwao 2-0 na Manchester City kwenye mkondo wa pili wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku.

Licha ya kupangwa kwenye kikosi cha wanasoka wa akiba, Mbappe, 22, hakuwajibishwa na PSG dhidi ya Man-City ugani Etihad kwa sababu ya jeraha la mguu. Ushindi uliosajiliwa na masogora wa Guardiola kwenye gozi hilo lilitosha kuwadengua PSG kwa jumla ya mabao 4-1.

“Tusitumie kutokuwepo kwa Mbappe kama kisingizio. Ukweli ni kwamba Man-City walicheza vizuri zaidi kuliko sisi. Nawapongeza Man-City ambao kusema kweli, wanajivunia msimu wa kuridhisha sana,” akaungama Pochettino – kocha raia wa Argentina aliyepokezwa mikoba ya PSG mnamo Januari 2021, miezi 13 baada ya kutimuliwa na Tottenham Hotpsur.

Bila Mbappe, PSG walishindwa kujipenyeza kwenye ngome ya Man-City waliojivunia pia safu thabiti ya ulinzi. Masogora wa Pochettino walizidiwa maarifa katika takriban kila idara huku fowadi wao tegemeo, Mauro Icardi, akishindwa kuelekeza kombora lolote langoni mwa wenyeji wao.

“Bila shaka kuwepo kwa Mbappe kungesaidia timu, hasa katika safu ya mbele ikizingatiwa utajiri wa kipaji chake. Hata hivyo, hatuwezi kulaumu hali hiyo ya kukosekana kwake kwa sababu kila mmoja kikosini alijituma kadri ya uwezo wake ila bahati ikakataa kusimama nasi na Man-City wakatumia vyema fursa walizozipata,” akasema Pochettino ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Southampton nchini Uingereza.

Chini ya Pochettino, Tottenham waliwahi kutinga fainali ya UEFA mnamo 2019 ila wakazidiwa ujanja na Liverpool.

Katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA dhidi ya Man-City, PSG walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya kiungo raia wa Senegal, Idrissa Gueye kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kikosi hicho kilijipata pia kikikamilisha mchuano wa mkondo wa pili na wanasoka 10 pekee uwanjani baada ya fowadi Angel Di Maria kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo kiungo na nahodha wa Man-City, Fernandinho.

Zikisalia mechi tatu pekee kwa kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu kukamilika rasmi, ni alama moja pekee ndiyo inawatenganisha viongozi wa jedwali Lille na PSG ambao wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 75.

Wakihojiwa mwishoni mwa mechi, wanasoka wa PSG, Ander Herrera na Marco Verratti walikiri kwamba refa Bjorn Kuipers alikuwa ameapa kuwaadhibu wakati wa mechi hiyo iliyowapa Man-City fursa ya kuweka hai matumaini ya kutwaa jumla ya mataji matatu ya haiba kubwa katika kampeni za muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Rais Kenyatta aalikwa awe mgeni wa heshima Tanzania...

Miaka yangu mitano kambini mwa Man-City sasa inaleta...