• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Ziara ya Suluhu ifufue uhusiano

TAHARIRI: Ziara ya Suluhu ifufue uhusiano

KITENGO CHA UHARIRI

ZIARA ya Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan humu nchini, ambayo ilikamilika jana, imeleta matumaini mapya ya kufufua uhusiano kati ya nchi hiyo na Kenya.

Mataifa hayo mawili yamekuwa na urafiki kwa muda mrefu, lakini kumekuwepo na changamoto wakati huo huo.

Matukio yaliyoashiria uhusiano mbaya hivi karibuni, yalishuhudiwa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais, marehemu John Pombe Magufuli.

Chuki iliyoanza kukita mizizi kati ya Wakenya na Watanzania hasa kupitia kwa mitandao ya kijamii ilihatarisha uhusiano mwema wa majirani.

Matukio kama vile kuchomwa kwa vifaranga waliokuwa wakisafirishwa kutoka Kenya kuelekea Tanzania, kuzuiliwa kwa mifugo waliovuka mpaka wakaingia Tanzania na hata kuhangaishwa kwa wanahabari Wakenya humo nchini, sasa yanafaa kusahaulika.

Rais Suluhu ameonyesha nia ya kustawisha uhusiano mwema kati ya mataifa haya mawili, na hiyo ni hatua bora.

Tungependa urafiki uliodhihirika wakati wa mikutano yote aliyohudhuria alipokuwa nchini udumu kwa muda mrefu, wala isiwe kwamba yote yalikuwa maonyesho ya kupumbaza raia wa mataifa hayo mawili pamoja na wadau wengine.

Kwa upande mwingine, Rais Uhuru Kenyatta ametangaza mabadiliko ya sera na sheria ambazo zitasaidia kuboresha uhusiano huu.

Mojawapo ya hatua kubwa iliyotangazwa na Rais Kenyatta ni kuruhusu Watanzania kufanya kazi humu nchini bila hitaji la kutafuta vibali vinavyotakikana kwa raia wa kigeni.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kuwa wananchi wa Kenya huenda wasifaidike sana na hatua hizi ikilinganishwa na jinsi wenzao Watanzania watakavyofaidi.

Ni matumaini yetu kwamba hatua hizi hazitafaidi Watanzania pekee, bali Wakenya nao watapata nafasi ya kufaidika kutokana na uhusiano mwema unaostawishwa kati ya mataifa hayo mawili.

Nchi zote za ukanda wa Afrika Kusini zina uwezo wa kupiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwa zitashirikiana, lakini kutoaminiana, ushindani kati ya baadhi ya viongozi na misimamo ya kupotosha kutoka nje husababisha vikwazo.

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuna sera nyingi ambazo huwa zimepitishwa kufanikisha maendeleo ya mataifa hayo yote yanayopakana lakini zimebaki kuwa maandishi kwenye karatasi kwani hakuna kinachotekelezwa kikamilifu.

You can share this post!

Kaunti kutumia zaidi ya 42m safari za nje

KINYUA BIN KING’ORI: Usawa wa kimaeneo utekelezwe...