• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Usawa wa kimaeneo utekelezwe tuachane na ukabila

KINYUA BIN KING’ORI: Usawa wa kimaeneo utekelezwe tuachane na ukabila

Na KINYUA BIN KING’ORI

MOJAWAPO ya manufaa makubwa ambayo Wakenya waliyatarajia kwa haraka kutokana na ujio wa katiba mpya ya 2010 ni kuleta usawa wa kimaeneo katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti katika nyadhifa zote muhimu.

Yaani haipaswi watu wa kabila moja au kaunti moja kushikilia nyadhifa muhimu serikalini na kutenga makabila mengine, na hilo likitokea itakuwa ni kosa na wahusika wakuu katika kufanya teuzi hizo watakuwa wamekiuka kipengele muhimu mno katika katiba ambayo wameapa kuilinda, kuitunza na kuitetea na kuhakikisha inatekelezwa ipasavyo.

Viongozi wanaotawala, ikiwa watavunja katiba kifungu cha uwakilishi wa usawa serikalini kikiwemo, wabunge ndio wanafaa kujitolea kulinda utekelezaji wa katiba kwa kukataa kuidhinisha teuzi zinazofanywa na serikali kwa kukiuka katiba.

Ninasema hivyo kwa sababu wabunge ndio wenye mamlaka ya kuwapiga msasa watu wanaopendekezwa kushikilia nyadhifa kuu na kuwaidhinisha ili kuteuliwa na Rais.

Mtindo wa watu kutoka kabila moja kuwa wakubwa katika asasi zote muhimu ni ukaidi wa katiba na unafaa kukomeshwa bila kupoteza muda zaidi.

Kuwa rais wa nchi au gavana wa kaunti hakumpi mtu kibali cha kuvunja katiba anayostahili kusimamia utekelezaji wake.

Ikiwa kuna serikali ambayo imeonyesha kutojali kuzingatia usawa katika kusambaza nyadhifa muhimu ni Jubilee yake Rais Uhuru Kenyatta.

Ikiwa kweli Rais Uhuru anayo nia njema katika azma yake ya kuhakikisha anatumia kipindi chake cha lala salama mamlakani kupalilia maridhiano nchini anafaa kuthibitisha hilo kwa kuonyesha usawa wa kimaeneo katika teuzi zinazofanywa na serikali yake.

Rais Uhuru anafaa kurejesha hadhi ya katiba yetu kwa kuweka ukabila kando na kukubali kuleta usawa na kukuza umoja na Ukenya wetu kwa kujaribu kujumuisha maeneo yote serikalini wakati wa kuajiriwa kupitia njia yoyote zikiwemo nyadhifa za kisiasa.

Suala hilo ni tatizo la kitaifa na Rais anafaa kulitatua kisiasa vinginevyo lawama atabeba yeye mwenyewe.

Ni unafiki wa hali ya juu viongozi wote wakuu nchini kuwa wametoka eneo la Mlima Kenya pekee.

Hii ni hatari na sijui kwa nini viongozi wa upinzani akiwemo Raila Odinga, Stephen Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi wametia pamba masikioni mwao na kujifanya hawasikii wala kuona upendeleo huu wa kikabila. Zile nguvu wanazotumia kila siku wakionekana kuwataka wabunge wa vyama vyao kuunga mkono mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI)!

Sasa wanafaa kufunguka macho na kuwataka wabunge hao kukataa kuidhinisha teuzi zinazochangia ukabila na kuvunja umoja wa nchi yetu ikiwemo uteuzi wa hivi majuzi uliofanywa na tume ya JSC kumpendekeza jaji mwenye tajriba pevu katika masuala ya kisheria Martha Koome kuwa rais wa idara ya mahakama ambapo Rais Uhuru tayari amewasilisha jina lake bungeni kuchunguzwa na kuidhinishwa.

Bunge lafaa kuwa mkombozi wa kuokoa uhai wa katiba kwa kuepuka kutumika kuinyonga katiba inavyonyongwa na asasi ya Rais. Utekezaji wa katiba na kugawa nyadhifa muhimu katika njia inayovutia sura ya taifa ndiyo njia tu inayoweza kuimarisha umoja, upendo na ushirikano na kuboresha uchumi.

Kupuuza katiba na kiongozi ni ukaidi, na kuonyesha kupendelea kabila fulani kunaweza kuleta maangamizi makubwa kwa uchumi wetu na kusaliti umoja wa taifa.

Nchi hii kiongozi anaweza kutoka kabila au eneo lolote, haiwi lazima rais awe kutoka Mlima Kenya, spika wa bunge awe kutoka Mlima Kenya, mwanasheria mkuu naye awe mzawa wa hukohuko Mlima Kenya, bila kujali tena anayeteuliwa katika idara ya mahakama awe kutoka Mlima Kenya.

Je, huo ndio usawa jamani?

Lengo la maoni haya si kupinga uteuzi wa kiongozi yeyote akiwemo dadangu yangu msomi Jaji Martha Koome lakini la muhimu hapa ni, uzalendo wetu uko wapi ikiwa tuko tayari kukubali idara zote muhimu serikalini ziongozwe na watu kutoka kabila au jamii moja tu.

Huu ndio wakati mwafaka wabunge wanafaa kuthibitishia wakenya wanastahili kuendelea kushikilia nyadhifa Zao Kwa kuzingatia Sheria, haki na umoja wetu wanapofanya maamuzi kuidhinisha watu wanaopendekezwa kushikilia nyadhifa muhimu serikalini, wazitumie tu Kwa maslahi ya kisiasa, katiba inafaa kupewa kipaumbele

You can share this post!

TAHARIRI: Ziara ya Suluhu ifufue uhusiano

KAMAU: Ndoa: Waafrika wajifunze kutokana na Wazungu