• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KAMAU: Ndoa: Waafrika wajifunze kutokana na Wazungu

KAMAU: Ndoa: Waafrika wajifunze kutokana na Wazungu

Na WANDERI KAMAU

CHANZO cha vifo vingi katika kizazi cha sasa ni ghasia zinazotokana na tofauti baina ya wanandoa.

Kila siku imegeuka kuwa ya majonzi. Majonzi yasiyoisha. Majonzi ya kuatua moyo na majonzi yanayozua hofu kuhusu mustakabali wa kizazi cha sasa.

Makumi ya vifo vya vijana wachanga sana vinaripotiwa karibu kila dakika baada ya kutofautiana na wapenzi wao.

Cha kusikitisha ni kuwa chunguzi zinapofanywa, inabainika kuwa baadhi ya sababu zinazowafanya wanandoa hao kutofautiana zinaweza kusuluhishwa kupitia mazungumzo.

Ingawa taasisi ya ndoa ilionekana kama chemchemi ya hekima miongoni mwa vizazi vya awali, hasa miongoni mwa Waafrika, dhana hiyo imebadilika.

Vijana wengi wanahofia kuingia kwenye ndoa, kwani inafasiriwa kama “njia ya mkato ya mauti”.

Hata hivyo, ni wakati mwafaka wa jamii kuhimizwa ichukulie suala hili kama janga kubwa na kuanza mikakati ya kusuluhisha mwekekeo huo wa kuhofisha.

Kwanza, ingawa mafundisho ya dini nyingi ni kuwa ndoa ni taasisi takatifu ambayo haipaswi kuingiliwa na yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, lazima fundisho hili litathminiwe upya.

Lazima mafundisho na dhana za kikale kuhusu ndoa ziwianishwe na maisha ya kisasa, ili kuepuka hali ambapo vijana wengi wanaendelea kupoteza maisha yao kwa kisingizio cha “kuzitetea ndoa zao”.

Hakuna jambo lolote lenye thamani kuliko maisha ya mwanadamu duniani. Hakuna!

Kulingana na mafundisho ya mwanafalsafa Aristotle, lengo kuu la kwanza la mwanadamu linapaswa kuwa, kuishi maisha yenye furaha. Anasema furaha na amani maishani ndizo nyenzo kuu zinazomwezesha mwanadamu kufikia ndoto zake.

Je, ni vipi tena kijana atashauriwa ahatarishe maisha yake kwa kukaa kwenye ndoa yenye changamoto tele ili “kutii” amri ya Mwenyezi Mungu?

Ikizingatiwa visa hivi vimekuwa vikishuhudiwa sana miongoni mwa jamii za Kiafrika, lazima Waafrika wajifunze kutokana na mielekeo ya masuala ya ndoa katika nchi za Magharibi kama vile Amerika.

Kwa mfano, Jumatatu, dunia nzima ilishangazwa na taarifa ya bwanyenye Bill Gates kutoka Amerika na mkewe, Bi Melinda Gates, kwamba wametalikiana baada ya kuoana kwa miaka 27.

Kwenye taarifa ya pamoja, walisema waliamua kufikia uamuzi huo baada ya kujaribu kusuluhisha tofauti zao bila mafanikio yoyote.

Mwelekeo huo umekuwa ukishuhudiwa miongoni mwa wanandoa wengi miongoni mwa Wazungu, ambapo huwa wanaamua kutalikiana ikiwa watashindwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Wanandoa wengine ambao walichukua mwelekeo huo ni bwanyenye Jeff Bezos na aliyekuwa mkewe, Bi Mackenzie Bezoz mnamo 2019, mwanamuziki Kanye West na mwanamitindo Kim Kardashian kati ya wengine.

Kinachoridhisha kwenye talaka hizi ni kuwa wanandoa huwa wanakubaliana kuhusu jinsi ya kuendelea kuwalea watoto wao na taratibu za kugawana mali waliyomiliki kwa kuwahusisha mawakili.

Inasemekana kuwa kutokana na idadi kubwa ya talaka nchini Amerika, kuna mawakili wengi wanaoendesha kesi hizo.

Licha ya wingi wa talaka, visa vya mauaji baina ya wanandoa katika nchi hizo huwa vichache sana, kwani kuna taratibu maalum ambazo huwa wanafuata.

Vivyo hivyo, imefikia wakati Waafrika wazinduke na kufahamu kuwa kila mwanadamu ana maisha yake hapa duniani, wala si lazima akwamilie kwenye ndoa ambayo haimfai.

Kila mmoja anapaswa kuishi maisha yenye furaha na amani.

[email protected]

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Usawa wa kimaeneo utekelezwe...

AKILIMALI: Kwa mtaji wa Sh40,000 pekee wanahesabu maelfu...