• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 1:50 PM
Manchester United kuvaana na Villarreal kwenye fainali ya Europa League

Manchester United kuvaana na Villarreal kwenye fainali ya Europa League

Na MASHIRIKA

LICHA ya Manchester United kupokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa AS Roma katika mkondo wa pili wa nusu-fainali ya Europa League mnamo Alhamisi usiku, kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kilifuzu kwa fainali ya muhula huu wa 2020-21 kwa jumla ya mabao 8-5.

Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kati ya saba zilizopita kwa Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kupoteza, na ni fainali ya kwanza kwa miamba hao kutinga chini ya Solskjaer ambaye ni raia wa Norway.

Edinson Cavani alifungia Man-United mabao yote mawili dhidi ya Roma kwenye mkondo wa pili wa nusu-fainali uliondaliwa nchini Italia.

Fowadi huyo raia wa Uruguay alifungulia Man-United ukurasa wa mabao kunako dakika ya 39 kabla ya kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 68 baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo raia wa Ureno, Bruno Fernandes.

Katikati ya muda wa kupatikana kwa mabao hayo ya Man-United, Roma walikuwa wamejitahidi kurejea mchezoni kupitia magoli ya Bryan Cristante na mfumaji wa zamani wa Manchester City, Edin Dzeko aliyefunga bao lake la tisa dhidi ya Man-United.

Roma ambao sasa watakuwa chini ya kocha Jose Mourinho kuanzia muhula ujao wa 2021-22, walifungiwa goli la tatu na Nicola Zalewski aliyemzidi ujanja beki Alex Telles na kumwacha hoi kipa David de Gea.

Ushindi wa jumla wa mabao 8-5 unatamatika nuksi iliyoshuhudia Man-United wakidenguliwa kwenye nusu-fainali nne zilizopita za mapambano tofauti. Masogora wa Solskjaer watanogesha sasa fainali ya Europa League msimu huu dhidi ya Villarreal ambao chini ya kocha Unai Emery, walibandua Arsenal ya kocha Mikel Arteta kwa jumla ya mabao 2-1. Fainali hiyo itatandaziwa mjini Gdansk, Poland mnamo Mei 26, 2021.

Man-United hawajawahi kujizolea taji lolote tangu 2017 walipowapiga Ajax ya Uholanzi na kutia kapuni ubingwa wa taji la Europa League. Huo ndio muda mrefu zaidi kwa kikosi hicho kushuhudia bila taji tangu 1985-1990 ambapo ukame wao wa mataji ulikomeshwa na kocha Sir Alex Fuerguson aliyewaongoza kunyanyua ufalme wa Kombe la FA.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kupepetana na Aston Villa mnamo Mei 9, 2021. Pambano hilo litakuwa mwanzo wa ratiba ngumu kwa masogora wa Man-United ambao watapiga jumla ya mechi tatu za EPL chini ya kipindi cha siku tano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wetang’ula awasaliti UhuRaila na msimamo wa OKA

Kocha Unai Emery azamisha matumaini ya Arsenal katika soka...