• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
WASONGA: Raila anaelekea kugeuza ODM chama cha kikabila

WASONGA: Raila anaelekea kugeuza ODM chama cha kikabila

Na CHARLES WASONGA

KUNG’ATULIWA kwa Mbunge wa Rarieda, wakili Otiende Amollo, kutoka wadhifa muhimu wa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Sheria (JLAC) kumethibitisha udikteta uliokolea ndani ya chama cha ODM.

Wa kulaumiwa kwa hali hii sio mwingine ila kiongozi wa chama Raila Odinga.

Kuna dhana potovu, haswa miongoni mwa wabunge fulani kutoka eneo la Nyanza, kwamba Bw Amollo na Seneta wa Siaya James Orengo walikosea; kwa kutia saini ripoti ya kamati ya pamoja ya sheria, iliyoharamisha maeneobunge mapya yaliyobuniwa na Mswada wa BBI.

Inasikitisha kuwa Bw Odinga anaamini ‘nadharia’ hii isiyo na mashiko.

Wabunge hao; John Mbadi (Suna Kusini), Junet Mohamed (Suna Mashariki) na Opiyo Wandayi (Ugunja), walidai kuwa Amollo na Orengo wanaendeleza azma ya mrengo wa Tangatanga unaotaka mswada huo wa marekebisho ya Katiba uangushwe katika mabunge yote mawili na kwenye referenda.

Katu sikubaliani na dhana hii. Watatu hao wanawapaka tope MaBw Amollo na Orengo kwa manufaa yao ya kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao 2022.

Wanataka kujipendekeza machoni mwa Bw Odinga ili wapate baraka zake kufanikisha ndoto zao za kushinda viti vya ugavana kwenye kaunti zao.

Ni siri iliyo wazi kwamba Mbadi anataka kutwaa kiti cha ugavana wa Homa Bay, ikizingatiwa kwamba Bw Cyprian Awiti anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

Naye Junet anatamani kiti cha ugavana wa Migori kwa kuwa Bw Okoth Obado anakamilisha muhula wake wa pili.

Sawa na Wandayi ambaye ametangaza wazi kwamba anataka kumrithi Gavana wa Siaya, Cornell Rasanga.

Sikubaliani na propaganda kwamba Bw Amollo alilenga kuhujumu Mswada wa BBI, kwa sababu ripoti iyo hiyo imewataka wabunge wapitishe mswada huo ulivyo licha ya kukiuka Katiba kwa kugawanya maeneo 70 yaliyopendekezwa.

Isitoshe, Bw Otiende aliposhiriki katika mjadala kuhusu mswada huo bungeni Alhamisi iliyopita, alifafanua kwamba japo ni kinyume cha Kipengele 89 cha Katiba kwa mswada kugawanya maeneobunge hayo miongoni mwa kaunti 28, Wakenya ndio wenye usemi wa mwisho kupitia kura ya maamuzi.

Hivyo, kwa mtazamo wangu wakili huyo hakukaidi msimamo wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta; kwamba wabunge wanapaswa kupitisha Mswada wa BBI ulivyo pasina kuufanyia marekebisho yoyote.

Hii ndio maana nashikilia kwamba MaBw Mbadi, Junet na Wandayi – ambao walikutana na Bw Odinga nyumbani kwake Karen majuzi – walimpotosha kinara huyo wa ODM kwamba Bw Amollo anazamisha jahazi la BBI.

Siasa chafu za wabunge hawa zimeshusha hadhi ya ODM na kuifanya kuonekana kama chama cha kikabila ilhali ni chama cha kitaifa.

Endapo Bw Odinga anataka Wakenya kuchukulia ndoto yake ya urais 2022 kwa uzito, akome kabisa kusikiza propaganda za wabunge wachache kutoa ngome yake ya Luo Nyanza ambazo zinaipaka tope sifa za ODM.

Kwa hakika kuondolewa kwa Bw Amollo kutoka kamati ya JLAC kutaikosesha kamati hii mchango muhimu wa mwanasheria huyo mwenye tajriba ya kipekee katika masuala ya kikatiba.

Mbunge huyo alikuwa mwanachama wa Kamati ya Wataalamu (CoE) walioandika Katibu ya sasa mnamo 2010.

You can share this post!

TAHARIRI: Refarenda isiwe ya kulazimishwa

MATHEKA: Kanuni za kuzuia maambukizi ya corona shuleni...