• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
MATHEKA: Kanuni za kuzuia maambukizi ya corona shuleni zikazwe

MATHEKA: Kanuni za kuzuia maambukizi ya corona shuleni zikazwe

Na BENSON MATHEKA

SHULE zinapofunguliwa Jumatatu, kuna mambo kadhaa ambayo wadau wanafaa kutilia maanani kuzingatia kwa usalama wa wanafunzi.

Ikizingatiwa hizi ni nyakati ngumu sana kutokana na hatari na athari za janga la corona, usalama wa wanafunzi na walimu wafaa kuzingatiwa hususan baada ya walimu kadha kufariki kutokana na maambukizi ya virusi hivyo.

Wamiliki wa shule za kibinafsi na maafisa wa Wizara ya Elimu mashinani – ambao ndilo jukumu lao kuzuru shule kukagua maandalizi ya utendakazi – pia wameripotiwa kuambukizwa corona na hata kufariki.

Wizara ya Afya imetoa kanuni za kuzuia msambao wa virusi hivi katika taasisi za elimu; iwapo zitazingatiwa kikamilifu, maambukizi shuleni yataepukwa.

Ukweli ni kwamba ingawa shule zinafunguliwa Jumatatu kulingana na ratiba ya Wizara ya Elimu, viwango vya maambukizi nchini vingali juu kama ilivyo nchi zingine.

Hii haifai kuwa kigezo cha kuendelea kufunga shule kama ambavyo baadhi ya watu wanapendekeza, kwani kutawanyima watoto nafasi ya kujikuza maishani.

Ukweli ni kwamba janga la corona litadumu ulimwenguni kwa muda, hivyo ni muhimu kwa kila nchi na jamii kutafuta mbinu za kujikinga.

Msingi wa mbinu hizi ni ushauri wa wataalamu wa afya, ambao wamekuwa wakifuatilia na kutafiti jinsi virusi hivi vinabadilika kote ulimwenguni; kupuuza ushauri wao ni kualika balaa.

Hivyo basi, usalama wa wanafunzi utaanzia nyumbani wazazi wakizingatia kikamilifu kanuni za afya na kuwafunza watoto wao jinsi ya kujikinga.

Katika shule za umma, serikali haina budi kuhakikisha kuna miundomsingi inayohitajika kuepuka msongamano madarasani.

Nao wasimamizi wa shule za kibinafsi hawafai kulegeza masharti kwa sababu ya tamaa ya pesa.

Visa vichache vya maambukizi vilivyoshuhudiwa muhula uliopita vinafaa kutoa funzo kwa wadau kuimarisha zaidi mbinu za kuzuia na kudhibiti maambukizi shuleni muhula huu wa tatu na siku zijazo.

Janga la corona limelemaza sekta nyingi lakini tunafaa kujifunza kukabiliana nalo siku baada ya siku kwani ni lazima maisha yaendelee.

Ikizingatiwa kwamba aina mpya za virusi na hatari zaidi zinaendelea kugunduliwa maeneo tofauti nchini, kuna haja ya kuhakikisha kwamba usalama umeimarishwa katika taasisi za elimu kwa kufanya hima kutekeleza kikamilifu kanuni zote za Wizara ya Afya.

Kupuuza ushauri wa wataalamu wa afya na kanuni zilizotolewa kutapepeta virusi hivi katika taasisi zetu za elimu.

You can share this post!

WASONGA: Raila anaelekea kugeuza ODM chama cha kikabila

KASHESHE: Walamba dili tamu