• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Hofu safari zikikwama Mto Athi sababu ya mamba

Hofu safari zikikwama Mto Athi sababu ya mamba

Na PIUS MAUNDU

HALI ya wasiwasi imeibuka miongoni mwa wakazi wa kaunti za Kitui na Makueni, baada ya mhudumu wa boti ambaye huwasaidia kuvuka Mto Athi katika kivukio cha Kitise-Katilini kushambuliwa na mamba.

Wenyeji hutumia kivuko hicho kwenda upande wa pili kazini, shambani, shuleni, sokoni na hospitali.

Kwa bahati nzuri mhudumu huyo Alex Musyoki alinusurika katika shambulio hilo.

Hata hivyo, alipoteza vidole vitatu na sasa hawezi kuendesha tena boti yake; hali ambayo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa majirani wake.

“Nilikodolea kifo macho. Nina bahati kuwa hai,” akasema Alhamisi kwenye mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake katika kijiji cha Katangini.

Ajali hiyo iliyofanyika wiki jana imeibua hofu kuhusu hatari inayowakumba wenyeji wanapovuka mto huo.

Hakuna daraja lililo karibu, hivyo bila huduma za boti hulazimika kuchelewesha mipango yao kwa hata wiki kadha hadi maji mtoni yapungue.

Njia mbadala ni kusafiri hadi mji wa Machakos ulio mbali kilomita 300, au mji wa Kibwezi mbali kilomita 100 ili kupata daraja la kuvuka.

Barabara iliyopendekezwa kujengwa ili kuunganisha kaunti hizo mbili pia huenda isiwafaidi.

Barabara hiyo inayotazamiwa kuwa yenye umbali wa zaidi ya kilomita 100 na kujumuisha daraja maalum la Thwake, inatarajiwa kugharimu Sh64 bilioni.

Wiki moja baada ya Bw Kativui kushambuliwa, mwanamume mwingine alizama mtoni na kuliwa na mamba.

Mwathiriwa, aliyetambuliwa kama Bw George Shiundu, alikuwa akihudumu kama mfanyakazi katika shamba moja eneo hilo.

Kulingana na chifu wa eneo la Kitise, Bw Patrick Murage, mabaki ya mwili wa mwendazake yalipatikana na wapiga mbizi wikendi iliyopita kwenye mto huo.

“Tumewaarifu jamaa zake na mipango ya mazishi tayari imeanza,” akasema.

“Ni jambo la kuogofya kuuvuka mto huo, hasa unapokuwa umejaa maji. Huwa ninatumia Sh100 kila siku kama ada ya kuvukia mto. Hiyo ni sehemu kubwa ya mapato yangu. Isitoshe, visa vya mashambulio ya mamba vimeongeza mzozo uliopo kuhusu usafiri,” aliongeza Bi Rachel Kamene ambaye hufanya kazi za vibarua eneo hilo.

“Tunaomba mvua iache kunyesha. Tunaiomba serikali pia ijenge daraja katika eneo hili,” akasema.

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Si lazima watu kukesha msikitini wakati...

Biashara zatarajiwa kunoga Iddi ikinukia