• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
MAKALA MAALUM: Corona ilipogonga riziki za wengi, ubunifu pekee ndio uliowaokoa

MAKALA MAALUM: Corona ilipogonga riziki za wengi, ubunifu pekee ndio uliowaokoa

Na SAMMY WAWERU

KENYA ilipokumbwa na ugonjwa wa Covid-19, mamia, maelfu na mamilioni ya wananchi walipoteza nafasi za ajira.

Kulingana na takwimu za serikali, zaidi ya watu milioni 1.72 wamepoteza kazi kufuatia athari za virusi vya corona, tangu kisa cha kwanza kiripotiwe nchini mnamo Machi 2020.

Sekta zinazohusisha mtagusano wa watu, kama vile ya hoteli na utalii, elimu, uchukuzi, ususi na ulimbwende, ni miongoni mwa zilizong’atwa kwa kiasi kikubwa na makali ya corona.

Paul Mwangi, 38, alikuwa akitoa huduma za urembo, ulimbwende na kunyoosha watu viungo vya mwili (Beauty Therapy & Reflexology).

Alikuwa ameajiriwa jijini Nairobi, na ni miongoni mwa waliopoteza kazi, kutokana na sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kusaidia kuzuia msambao zaidi.

Aidha, anasema ni shughuli aliyokuwa amefanya kwa zaidi ya miaka 10.

“Kwa sababu ya wateja kuogopa kuambukizwa virusi vya corona, biashara katika maduka ya kurembesha ilizorota, wengi wetu tukaenda nyumbani,” Mwangi anasimulia.

Ni mume na baba wa watoto wawili, hivyo basi hakuwa na budi ila kujikaza kisabuni kukidhi familia yake kwa riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Akiwa mzaliwa wa Kinangop, Kaunti ya Nyandarua, alilelewa katika mazingira ya kilimo, na anasema baada ya kuwaza na kuwazua, alikumbatia shughuli za zaraa kama njia mbadala ya kujiendeleza kimaisha.

“Nilikuwa nimeweka akiba ya pesa kiasi nikiwa kazini na ndizo nilizotumia kuingilia kilimo,” anasema.

Ana ekari mbili za shamba, na alitenga nusu ekari kukuza viazimbatata.

Anafichua kwamba alitumia mtaji wa Sh75,000 kukuza viazi ambavyo miezi minne baadaye vilimuingizia Sh125, 000.

“Mazao yalikuwa ya kuridhisha, nilivuna jumla ya magunia 50 niliyouza Sh2,500 kila gunia,” anafichua, akiongeza kuwa faida aliyopata ilimchochea kuendeleza kilimo.

Nusra akate tamaa baada ya Nairobi kufungwa: Mwangi pia anasema alikuwa ameandaa jukwaa la upanzi wa miche 6,000 ya kabichi.

Amri ya ama kuingia au kutoka Kaunti ya Nairobi na viunga vyake, ambavyo ni soko kuu la mazao ya kilimo, iliyotekelezwa kati ya mwezi Aprili na Julai 2020, nusra izime jitihada zake.

“Niliuza kabichi 300, kila kipande kikinunuliwa kwa Sh5 pekee. Mazao mengine yaliozea shambani na kuliwa na mifugo kwa sababu ya kikwazo cha usafiri na uchukuzi, kupeleka mazao Nairobi,” anasema, akikadiria hasara.

Hata hivyo, Mwangi hakufa moyo, kwani alifahamu bayana hakuwa na tegemeo lingine la kuzimbulia familia yake riziki. Mbali na viazi na kabichi, alijumuisha karoti na maharagwe asilia ya kijani (garden peas).

Wakati wa mahojiano, mkulima huyo alisema kwa sasa anakuza mseto huo wa mimea katika jumla ya ekari mbili.

Alisema mazao ya karoti aliyokuwa nayo shambani yalikutana na bei kati ya Sh1,500 – 3,000 gunia la kilo 130, huku kilo moja ya maharagwe asilia maarufu kama minji ikiwa kati ya Sh30 -Sh150.

Ameratibu shamba lake, viazi anavilima kwenye ekari moja, kisha kabichi, karoti na minji katika ekari moja na nusu, kila mmea kipande chake.

Mwangi anategemea maji ya mvua. “Ninaendelea kujipanga niweze kununua mifereji na vifaa vya kunyunyizia mimea na mashamba maji,” akaambia Taifa Leo.

Shughuli za kilimo anaziendeshea katika kijiji cha Yaang’a, karibu na Mji wa Njabini, eneo la Kinangop. Kwa sasa ana viazi vinavyoendelea kukua.

Mkulima huyo anasema kikwazo kikuu katika kilimo cha viazimbatata ni ukosefu wa mbegu bora na zilizoafikia ubora.

“Hakuna mbegu halisi zilizoidhinishwa ili kuboresha kilimo cha viazi,” anasema.

Changamoto nyingine zinazomkabili sawa na wakulima wengine eneo la Kinangop ni miundomsingi duni ya barabara, akisema msimu wa mvua huwa anatatizika kusafirisha mazao sokoni.

“Bei ya fatalaiza na pia dawa za wadudu inaendelea kuwa ghali. Serikali iitathmini ili kuokoa wakulima,” Mwangi aihimiza serikali.

Huduma tamba za hoteli jijini

Katika kitovu cha jiji la Nairobi (CBD), tunakutana na Daisy Mwende ambaye anafanya huduma tamba za mkahawa.

Licha ya kuwa sekta ya mikahawa na utalii inaendelea kukadiria hasara, ikizingatiwa kuwa imepoteza idadi ya juu ya wafanyakazi, Mwende ameamua kujiajiri kupitia usambazaji wa vyakula jijini.

Ni mpishi hodari wa vyakula asilia kama vile mukimo, githeri, nduma, ugali, minji na samaki. Mwanadada huyu pia huandaa pilau, chapati, mboga za kienyeji, kati ya vyakula vinginevyo, ambapo mbali na Nairobi – CBD – pia husambaza katika mitaa ya kifahari kama Upper Hill, Hurlingham, Ngong Road na Buruburu.

“Wateja wangu ni walioko kwenye ofisi, huwasaidia kuokoa muda kuenda hotelini na pia kuwapunguzia gharama ya juu ya mlo jijini,” Mwende anaelezea, akisema bei ya vyakula vyake ni kati ya Sh200 – 400.

Daisy Mwende akiwa jijini Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Huku maelfu na mamilioni ya watu walioathirika kutokana na corona wakikuna kichwa jinsi watakavyoweza kujiendeleza kimaisha, Mwende, 25, anasifia kazi anayofanya akisema kuwa inamsaidia kukimu mahitaji yake ya kimsingi.

Ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka tisa. Mwende pia ni mwanafunzi wa kozi ya uhasibu.

“Kimsingi, ninapenda shughuli za mapishi. Niligeuza mapenzi hayo kuwa biashara 2019, japo nikasitisha baadaye kwa muda nilipojiunga na chuo,” anafafanua.

Anafichua kuwa alitumia mtaji wa Sh10,000 pekee kuanza huduma tamba za hoteli.

“Nimejifunza mengi kutokana na janga la Covid-19. Badala ya kuendelea kutegemea ajira ambazo hazipatikani, tunapaswa kuibuka na suluhu sisi wenyewe kwa kubuni nafasi za kazi,” Mwende anashauri, akisema ana vibarua wawili wanaomsaidia kusambaza vyakula.

“Changamoto zipo, bei ya bidhaa za mapishi inazidi kuwa ghali na ni muhimu serikali ibuni sheria na mikakati maalum kuidhibiti,” aomba. Akiendelea kupalilia biashara hiyo, anasema kwa siku huhudumia wastani wa wateja 20. Anasema ipo siku atafungua mkahawa wa kifahari unaoandaa vyakula vyenye asili ya kienyeji,

Mwalimu aamua kuuza matunda: Pauline Nyaguthii, mwalimu katika Shule ya Kibinafsi ya Kiangai Blessings View Academy, Kaunti ya Kirinyaga, baada ya mkurupuko wa corona nchini, Machi 2020, aliingilia biashara ya bidhaa za kula.

“Walimu wa shule za kibinafsi ni kati ya waliohangaika, na sikuwa na budi ila kutafuta ila njia mbadala kusaka riziki. Nilianza uuzaji wa matikitimaji, machungwa, karakara na bidhaa zingine mbichi za shambani,” Nyaguthii ambaye ni mama wa mtoto mmoja anaelezea.

Covid-19 ni janga la kimataifa lililotoa funzo kwa wengi. Nicholas Njiru ambaye alikuwa katika sekta ya utalii anakiri mambo yalipogonga mwamba kilimo kilimsimamia.

Hukuza nyanya na vitunguu eneo la Mai Mahiu.

“Licha ya kuwa nimerejelea kazi ya kusafirisha watalii, kilimo kiliniajiri kipindi ambacho maisha yalikuwa magumu,” Nicholas ambaye ni mmiliki wa Quick Link Tours & Travel, alisema.

Kwa upande wake, Paul Mwangi, alipoulizwa endapo atarejea katika sekta ya urembo na ulimbwende Kenya ikishinda vita dhidi ya Covid – 19 alijibu: “Kilimo kimethibitisha kuwa tegemeo kuu, hususan majanga yanapoibuka. Nimekigeuza kuwa afisi yangu ya kila siku, kozi niliyosomea huenda ikawa kazi ya ziada siku za usoni.”

Mkulima huyo anasema ni kupitia shughuli za kilimo ambapo ameweza kujiondoa kwenye orodha ya mamia, maelfu na mamilioni ya waliopoteza ajira.

Dennis Muchiri, mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi, anasema ni muhimu kuweka akiba unapokuwa kazini kwa minajili ya siku za usoni.

“Janga la Covid-19 limefungua wengi mawazo, haja ya kuweka akiba na kuwekeza katika kazi inayoingiza pato la ziada. Ni muhimu kujiunga na chama cha ushirika (Sacco) au shirika la kifedha kama vile benki kuweka akiba, ili kuchukua mikopo kujiimarisha kimaendeleo,” Muchiri ashauri.

 

 

 

 

You can share this post!

Serikali yasisitiza kufungua shule Jumatatu

MAKALA MAALUM: Mambo kwa ‘ground’ si mzaha, Wakenya...