• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
MUTUA: Ndoa, talaka na fumbo linaloitwa mapenzi

MUTUA: Ndoa, talaka na fumbo linaloitwa mapenzi

Na DOUGLAS MUTUA

KUMBE matatizo ya wanaume – na wanawake vile vile – ni mamoja kote duniani?

Kumbe ndoa, ya kizungu au kiafrika, ni ndoa tu?

Ni nadra kwangu kuandika kuhusu visa vya mahusiano, lakini hiki cha bwanyenye wa kimataifa, Bill Gates, kumtaliki mkewe, Belinda, kimenisadikisha kukiandikia.

Kisa na maana ni kwamba kwanza, kinahusisha mafedha ya kutupwa. Pili, masaibu yaliyoisibu ndoa hiyo ni yale yale yanayoikumba ya kina pangu-pakavu-tia-mchuzi kule kwenu kijijini.

Japo tumeambiwa tangu zamani kwamba pesa ni sabuni ya roho, sabuni yenyewe imeshindwa kutakatisha roho katika visa ambapo mihimili ya ndoa imetikiswa.

Kilichonivutia zaidi kuhusu talaka ya Bill na Belinda ni makubaliano yao kabla ya kuoana mnamo 1994.

Labda kutokana na wingi wa mafedha yake, Bill alifanikiwa kumshawishi Belinda amruhusu kuwa na faragha ya angaa siku tatu hivi kila mwaka na aliyekuwa mpenzi wake, Ann Winblad. Unaweza tu kukisia yaliyokuwa yakiendelea huko faraghani.

Mume wa watu, baba wa watoto wanne, anawezaje kwenda ‘mafichoni’ na aliyekuwa mpenzi wake kwa ruhusa ya mkewe?

Ikiwa huna mafedha usinijibu. Nadhani huelewi kabisa pesa ni mvunja mlima.

Lakini sikulaumu kabisa. Hata kwa mtazamo wa kimarekani, huo ni mpango wa ajabu sana hasa kwa watu ambao bado hawajaelewa ushawishi wa pesa.

Kwa mfano, Bill alipata idhini ya Ann kumuoa Melinda. Ni wanawake wangapi Afrika wanaoweza kuwasikiliza wapenzi wao wakiwaambia: ngoja nimuulize aliyekuwa mpenzi wangu iwapo ninafaa kukuoa? Kumbuka kuna matrilioni ya shilingi hapa.

Pesa na sifa ni mseto muovu ambao hushawishi watu kufanya mambo ya ajabu sana, kwa sababu hakuna anayetaka kuponyokwa na utajiri wala umaarufu.

Hatujui kwa hakika kilichosababisha talaka ya Bill na Melinda, lakini tutajua tu kwani hakuna linalojificha milele Marekani. Wadaku nchini humu wanaweza kujaa mji!

Ni kwa sababu ya pesa na umaarufu ambapo hata katika jamii zetu za Afrika mahusiano ya ajabu huendelea kimyakimya hadi pale tatizo litakapotokea, wadau wapasue mbarika.

Unaweza kukifananisha kisa cha Bill na Melinda na kile cha mchekeshaji wa kipindi cha Churchill Live, Profesa Hammo, na nyumba yake ndogo, Jemutai.

Uhusiano wa kimapenzi kati ya wachekeshaji hao uliendelea kwa muda mrefu, sikwambii pakazaliwa na watoto wawili, hadi pale pesa zilipopungua. Ninailaumu corona!

Ulionishangaza ni muafaka wao; ambapo msaada wa kuwalea watoto wa Profesa Hammo (Herman Kago) na Jemutai, hutumiwa Jemutai na mke wa Hammo. Inawezakanaje?

Mpango wa Bill kwenda faragha na Ann haukunishtua sana kwani ninaelewa ni kinyume cha sheria kwa mtu kuoa wake wengi Marekani. Haiwezekani, utafungwa jela!

Hivyo, wanaume na tamaa yao, hasa wakiwa na mafedha, huzalisha huku na kule wakabaki na jukumu la kulea.

Nisiyoelewa ni sababu ya Wakenya wanaojiweza kuwa na mipango ya aina hii ya malezi, ilhali sheria inawaruhusu kuoa wake wengi. Labda ni mbinu ya kuyakimbia majukumu mengi tu yanayoambatana na ndoa.

Yote tisa, kumi ni kwamba katika suala hili kuna vitu viwili vya kutunza: afya na moyo wako.

[email protected]

 

You can share this post!

Mombasa yatoa kanuni za sherehe za Idd kuzuia maambukizi

Tangatanga wamsaliti Ruto