• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Solskjaer alia ugumu wa ratiba ya Man-United watakaopiga mechi sita chini ya siku 17

Solskjaer alia ugumu wa ratiba ya Man-United watakaopiga mechi sita chini ya siku 17

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amelalamikia ugumu wa ratiba iliyoko mbele yao kwa kusema kwamba waratibu wa baadhi ya michuano ya soka ya Uingereza ni “watu ambao hawajawahi kucheza kabumbu katika maisha yao yote.”

Man-United walitinga fainali ya Europa League msimu huu kwa kuwadengua AS Roma kwa jumla ya mabao 8-5 mnamo Mei 6, 2021.

Hata hivyo, kikosi hicho kwa sasa kitalazimika kutandaza jumla ya michuano sita chini ya kipindi cha siku 17 zijazo.

Baada ya kumenyana na Aston Villa ugenini mnamo Mei 9, Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamepangiwa kuchuana na Leicester City ugani Old Trafford mnamo Mei 11.

Gozi la EPL lililoahirishwa kati yao na Liverpool ugani Old Trafford sasa litapigwa Mei 13, siku nne kabla ya masogora wa Solskjaer kualika Fulham kwa ajili pambano jingine la EPL uwanjani Old Trafford. Baadaye, kikosi hicho kitapepetana na Wolves ugenini mnamo Mei 23 kabla ya kushuka dimbani kupimana ubabe na Villarreal ya Uhispania kwenye fainali ya Europa League mnamo Mei 26.

Solskjaer ambaye ni raia wa Norway, anahisi kwamba ugumu wa ratiba mbele yao itachangia mavune na uchovu wa kikosi chake pamoja na kuwaweka masogora wake katika hatari ya kupata majeraha mabaya yatakayowaweka nje kwenye fainali zijazo za Euro na hata mwanzo wa msimu ujao wa 2021-22.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Matiang’i awajibu maseneta kuhusu kukamatwa kwa...

ODM iko imara, tayari kutwaa urais – Sifuna