• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Lille wakomoa Lens na kuweka mkono mmoja kwenye taji la Ligi Kuu ya Ufaransa

Lille wakomoa Lens na kuweka mkono mmoja kwenye taji la Ligi Kuu ya Ufaransa

Na MASHIRIKA

LILLE walianza kunusia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu kwa mara ya kwanza tangu 2011 baada ya kuwatandika Lens 3-0 mnamo Ijumaa.

Burak Yilmaz alifungulia Lille ukurasa wa mabao katika dakika ya nne kupitia penalti kabla ya Lens kusalia uwanjani na wachezaji 10 pekee baada ya Clement Michelin kufurushwa uwanjani kwa kuonyeshwa kadi mbili za manjano chini ya kipindi cha dakika 35.

Lille walichuma nafuu kutokana na uchache wa wageni wao uwanjani na kufunga bao la pili kupitia kwa Yilmaz katika dakika ya 40 kabla ya Jonathan David kuzamisha kabisa chombo cha Lens kunako dakika ya 60.

Zikisalia mechi mbili pekee kwa kampeni za Ligue 1 msimu huu kutamatika rasmi, Lille wanajivunia alama nne zaidi kuliko Paris Saint-Germain (PSG) ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza dhidi ya Rennes ili kufikia idadi ya mechi 36 ambazo zimesakatwa na Lille.

Lille walitawazwa wafalme wa Ligue 1 kwa mara ya mwisho miaka 10 iliyopita na wanalenga kuwa kikosi cha pili baada ya AS Monaco mnamo 2016-17 kukomesha ukiritimba wa PSG katika soka ya Ufaransa tangu 2013.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kampuni ya Mumias mbioni kurejelea usagaji wa miwa

Mashambulio yatokea Afghanistan kipindi Amerika iko mbioni...