• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Korti yafungua miradi ya mabilioni ya pesa Pwani

Korti yafungua miradi ya mabilioni ya pesa Pwani

NA BRIAN OCHARO

UTEKELEZAJI wa miradi ya mabilioni ya pesa inayolenga kukabiliana na tatizo la ukame katika eneo la Pwani utaendelea licha ya kuibuka kwa madai ya ufisadi wakati wa mchakato wa ununuzi na utoaji wa zabuni.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu ya Mombasa kutupilia mbali ombi la shirika la kupigania haki za binadamu ambalo lilitaka miradi hiyo isimamishwe.

Jaji Mkazi Eric Ogola alitupilia mbali kesi hiyo akisema haikuibua masuala yoyote ya kikatiba yanayoweza kumfanya asimamishe miradi hiyo.

Miongoni wa miradi hiyo ni uwekaji wa bomba kwa umbali wa kilomita 100, kuchimba visima vya maji, ujenzi wa mabwawa na matangi ya kuhifadhi maji safi ya kunywa kaunti za Kilifi, Kwale, Tana River, Taita –Taveta na Lamu. Miradi hiyo ikadiriwa kugharimu zaidi ya Sh1.86 bilioni

“Mlalamishi ameshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kama invyotakikana kisheria. Kesi hii haina uzito na hivyo basi imetupiliwa mbali, ” akasema jaji.

Wakfu wa Coast Legal Aide and Resource Foundation (CLARF) ulikuwa umeshtaki Mamlaka ya Maendeleo ya Huduma za Maji Pwani,(CWWDA) Mwanasheria Mkuu Kariuki Kihara, na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma.

Shirika hilo pia lilitaka kuzuia Hazina ya Kitaifa kutoa fedha za miradi hiyo.

CLARF ilipinga mchakato wa ununuzi na kutaka kupewa stakabadhi zinazoonyesha majina ya kampuni zilizopewa zabuni ya miradi hiyo.

Lakini CWWDA ilikataa kuwasilisha stakabadhi hizo. Shirika hilo lilielekea mahakamani kulazimisha CWWDA kutoa stakabadhi hizo huku likidai ukiukaji wa haki ya kupata taarifa kutoka kwa afisi za umma.

CLARF lilishutumu CWWDA kwa kupuuza mchakato wa zabuni kwa kushindwa kuthibitisha, kupitia tangazo, jina la kampuni iliyoshinda zabuni hiyo.

“CWWDA ilipuuza na kukataa kutoa majina ya kampuni zilizopewa zabuni hizo,” alisema Bw Joseph Juma.

Bw Juma alidai zaidi kuwa mchakato wa ununuzi ulifanywa kwa siri kwa kiwango ambacho asilimia 10 ya jumla ya mkataba ilitolewa bila nyaraka halali.

“Umma ulinyimwa nafasi ya kuwahoji washiriki katika mchakato wa ununuzi na zabuni hiyo. Kwa hivyo, walipa ushuru huenda wakapoteza pesa kwa wanakandarasi hao,” Bw Juma ambaye ni mwakilishi wa CLARF alisema.

Aliiambia korti kuwa majaribio kadhaa ya shirika hilo kupata stakabadhi za zabuni hizo ili kuiwezesha kuipinga mahakamani yalipuuzwa .

Shirika hilo, hata hivyo, lilisema kwamba lilifuata utaratibu unaostahili wakati wa kutoa zabuni za miradi hizo.

CWWDA ilisema ilichapisha mwaliko wa umma kwenye mtandao wake na kufungua zabuni zilizopokelewa mbele ya wazabuni wote waliochagua kuhudhuria.

“Kulingana na pendekezo la Kamati ya Tathmini ya Zabuni, zabuni ilipewa kampuni zilizofanikiwa na wale waliohusika katika zoezi hilo walijulishwa ipasavyo,” Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa shirika hilo Jacob Torrut alisema, akiongeza kuwa ripoti juu ya ununuzi uliofanywa ilichapishwa.

Pia, Bw Torrut aliweka wazi kuwa miradi mingine tayari imekamilika, wakati mingine mikubwa bado inaendelea na malipo yao tayari yamefanywa , kwa hivyo malalamishi yoyote yanapaswa kuelekezwa kwa Bodi ya Ukaguzi wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma.

Jaji Ogola alibaini kwamba mlalamishi alipaswa kutoa barua aliyoiandikia shirika hilo, akiomba habari hizo, kwa mahakama kuthibitisha usahihi wake.

“Hata kama CWWDA lilikataa kutoa stakabadhi hizo, mlalamishi bado angejaribu njia nyingine za kutatua mzozo huo kabla ya kuelekea mahakamani kushtaki,” alisema Jaji Ogola.

Kulingana na mahakama , hakuna ukiukaji wa haki za kupata habari uliothibitishwa dhidi ya CWWDA.

You can share this post!

JAMVI: Ukimya uliogubika OKA ni ishara mbovu, Uhuru...

MALENGA WA WIKI: Tungo za Muyaka zilikuwa chachu ya...