• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
WANTO WARUI: Serikali iokoe wanafunzi wanaotaabika Mbeere Kusini

WANTO WARUI: Serikali iokoe wanafunzi wanaotaabika Mbeere Kusini

NA WANTO WARUI

HUKU shule zikifunguliwa hii leo, wanafunzi kutoka familia maskini hawana uhakika wa kurudi shuleni kutokana na taabu inayokumba jamii zao eneo la Makima, Mbeere Kusini katika kaunti ya Embu.

Familia hizi ambazo zilihamishwa kutoka katika vijiji vya Ndunguni, Mwanyani na Makima na Shirika la TARDA sasa hazina makao na zimejitafutia afueni ya muda katika shule za msingi na sekondari za Ndunguni.

Kwa mujibu wa watu hawa, shirika la TARDA liliwahamisha kwa nguvu kutoka ardhi wanayodai ni yao na ambako wameishi kwa zaidi ya miaka hamsini tangu mwaka wa 1968.

Shirika la TARDA kwa upande wake linadai kuwa ardhi hiyo ni yake na wamehamisha watu ili wapanue maendeleo katika mabwawa ya Masinga na Kamburu.

Hata hivyo, kuhamisha familia nyingi kiasi kile bila kuzielekeza pa kukaa ni kosa. Ni makosa zaidi hasa wakati huu ambapo nchi yetu na ulimwengu kwa ujumla tunakumbwa na mkurupuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Kwa sasa watu hawa wamebanana pamoja kama wanyama bila kuzingatia maagizo tunayopewa na Wizara ya Afya ya kukaa mbali na watu, kunawa mikono na kuvaa barakoa.

Hali waliyomo wanafunzi wa familia hizi ni tete na hawajui watafanya nini huku wenzao kote nchini wakirudi shuleni. Si hayo tu, hawana chakula na maji na wanaishi na kulala katika baridi kuu kwa neema za Mungu tu. Je, ugonjwa wa Covid-19 ukiingia katika sehemu kama ile itakuwa vipi? Ni nani ataweza kugharimia matibabu ya watu wale?

Mpango

Ikiwa ni kweli ardhi ile ini ya TARDA na watu hao wameishi huko kwa zaidi ya miaka hamsini kama wanavyosema, basi shirika hilo lilistahili kushirikiana na serikali na kufanya mpango maalumu wa kuhamisha watu hao huku wakioneshwa mahali mbadala pa kuishi bali si kufurushwa kiholela tu.

Mara kwa mara Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akikariri kuwa jukumu kuu la serikali ni kulinda maisha ya wananchi wake kwanza kisha mali yao.Kutokana na usemi huu wa Rais ambao kwa hakika ni sehemu ya Katiba yetu, basi kuna haja kubwa serikali iingilie kati na kusaidia familia hizi ambazo hazina makao.

Aidha, serikali ya Kaunti ya Embu inahitaji kuwajibika kwa haraka kutatua tatizo hili kwani kuna wanafunzi wengine pia wa sehemu hizo ambao wanahitajika kurudi shuleni. Je, wanafunzi hawa wataenda kusomea wapi?

Ni makosa makubwa kwa shirika lolote au watu binafsi kuhamisha watu kiholela. Serikali ihakikishe kuwa wanafunzi wa familia hizi ambao wanahitaji kurudi masomoni wametafutiwa shule za kusomea na mahali pazuri pa kuishi!

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Hakuna mwananchi mdogo wala mkubwa

Majonzi watoto 60 waliokufa kwenye shambulio wakizikwa