• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Majonzi watoto 60 waliokufa kwenye shambulio wakizikwa

Majonzi watoto 60 waliokufa kwenye shambulio wakizikwa

Na AFP

IDADI ya wasichana wa shule waliofariki mabomu yalipolipuka nje ya shule yao katika eneo wanakoishi Waislamu wa Shia jijini Kabul, imefika 60 huku miili yao ikizikwa jana katika makaburi yaliyopo mlimani jijini humo.

Mabomu kadhaa yaliyolenga shule ya wasichana yalilipuliwa Jumamosi katika moja ya mashambulizi mabaya nchini Afghanistan kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Wasichana zaidi ya 100 walijeruhiwa katika shambulio hilo eneo la Dash-e-Barchi, magharibi mwa Kabul.Serikali ililaumu kundi la Taliban kwa shambulio hilo lakini lilikanusha kuhusika.

Shambulio hilo lilijiri huku jeshi la Amerika likiendelea kuondoa wanajeshi wake wa mwisho wapatao 2,500 kutoka nchi hiyo iliyoharibiwa na ghasia licha ya juhudi za kupatanisha Taliban na serikali ya Afghanistan.

Msemaji wa wizara ya usalama wa ndani, Tareq Arian, aliambia wanahabari kwamba bomu la kwanza lilipuka katika lango la shule ya Sayed Al-Shuhada na wakati wanafunzi walikimbia nje, mabomu mengine mawili yalilipuka.

Alisema kwamba zaidi ya watu 100 walijeruhiwa wengi wao wakiwa wanafunzi wasichana.Wakazi walikuwa katika pilkapilka za kununua bidhaa kwa maandalizi ya siku kuu ya Eid al-Fitr, kuadhimisha mwisho wa Ramadhan.

Mnamo Jumapili, jamaa walianza kuzika miili katika makaburi yaliyo kwenye mlima yanayofahamika kama makaburi ya mashahidi.Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo lakini maafisa wa Afghanistan akiwemo Rais Ashraf Ghani walilaumu Taliban.

“Kundi hilo la uharibifu halina nguvu za kukabiliana na vikosi vya usalama vitani na badala yake linalenga taasisi za umma na shule za wasichana kwa ukatili,” Ghani alisema baada ya milipuko hiyo.

Kundi hilo limekanusha kwamba lilihusika na kusisitiza kuwa halijatekeleza mashambulizi Kabul tangu Februari mwaka jana walipotia saini mkataba na Amerika uliotoa nafasi ya mazungumzo ya amani na kuondolewa kwa wanajeshi wa Amerika waliosalia Afghanistan.

Kila siku, kundi hilo limekuwa likipingana na maafisa wa usalama wa Afghanistan katika nchi hiyo huku Amerika ikiendelea kuondoa wanajeshi wake.

Amerika ilipaswa kuwa imeondoa wanajeshi wake wote nchini humo kufikia Mei 1 chini ya mkataba wake na Taliban mwaka jana, lakini ikaongeza muda hadi Septemba 11, hatua ambayo iliwakasirisha wanamgambo hao.

Balozi wa Amerika jijini Kabul, Ross Wilson, alitaja shambulio la Jumamosi kama ukatili usioweza kusamehewa. “Shambulio hili dhidi ya watoto lisiloweza kuvumiliwa, ni shambulizi kwa hali ya baadaye ya Afghanistan,” Wilson alisema kwenye Twitter.

Eneo la Dasht-e-Barchi limekuwa likilengwa kwa mashambulizi na wapiganaji wa Waislamu wa Sunni.Mnamo Mei mwaka jana, kundi la wanaume waliokuwa na bunduki lilishambulia hospitali mchana na kuua watu 25 wakiwemo akina mama 16 waliokuwa wamejifungua.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali iokoe wanafunzi wanaotaabika Mbeere...

Spika atangaza nia ya kumrithi Gavana Mutua