• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KONDOO WA RUTO MATAANI

KONDOO WA RUTO MATAANI

Na CHARLES WASONGA

Wanachama wa vuguvugu la Tangatanga wanajitokeza kama kondoo wasio na mchungaji baada ya Naibu Rais William Ruto kuwaacha mataani kwa kukosa kuwapa mwelekeo wa pamoja kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI.

Wabunge wanaomuunga mkono walikiri kwamba, hakuwapa mwelekeo thabiti wakati mswada huo ulipopigiwa kura bungeni Alhamisi.Wengine walishawishiwa na masilahi ya kaunti wanakotoka baada ya kupata nyongeza ya maeneobunge pamoja na kuongezwa kwa mgao wa mapato kwa serikali za kaunti.

Hii ni licha ya wabunge hao awali kuapa kuangusha mswada huo wakidai mchakato huo sio jambo la dharura wakati huu.Wakati wa mjadala kuhusu mswada huo, wabunge hao walisema jambo la dharura wakati huu ni kupatikana kwa chanjo ya Covid-19 na ufufuzi wa uchumi.

Mnamo Alhamisi, Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, ambaye ni mwandani sugu wa Dkt Ruto, aliwashangaza wengi alipopiga kura ya kuunga mkono Mswada wa BBI akijitetea kuwa alifikia uamuzi huo kwa sababu unapendekeza kuiongezea Nakuru maeneo bunge matano zaidi.

“Sikushawishiwa na yeyote kupiga kura nilivyofanya na hiyo haimaanishi nilimsaliti Naibu Rais. Mswada huu unaifaa kaunti ya Nakuru na nitaendelea kumuunga mkono Ruto katika azima yake ya kuwania urais,” akasema kupitia taarifa katika ukurasa wake wa Facebook.

Siku moja baada ya jumla ya wabunge 235 kupitisha mswada huo huku 83 wakipinga, Dkt Ruto alikubali uamuzi huo na kuhimiza uheshimiwe kwa sababu ulikuwa wa kidemokrasia.

“Kwa sababu ni asasi ya kidemokrasia, Bunge la Kitaifa lilipigia kura Mswada wa Mageuzi ya Katiba na Seneti itafanya hivyo. Nafasi ya wananchi itakapojiri wao pia watapiga kura na tutaendelea mbele. Twapaswa kuheshimu uamuzi wa kila mtu na kukubali matokeo ya shughuli ya kidemokrasia; maoni yote yanaimarisha umoja wetu.” akasema katika ujumbe wake kupitia Twitter.

Wadadisi wanasema kauli hii ya Naibu Rais, inaashiria kuwa aliwaachilia wabunge wandani wake bila kuwaagiza wapige kura ya la kwa mswada huo wa BBI, ilhali mrengo wa handisheki ulishawishi wabunge wao kupiga kura ya kuunga Naibu Rais.

Alisema haya dakika chache baada ya wabunge wa mrengo wa Kieleweke, wakiongozwa na kiongozi kiongozi wa wengi Amos Kimunya, kudai matokeo hayo yanaashiria “kifo cha mrengo wa Tangatanga na mazishi yake yatafanyika 2022.”

“Kupitishwa kwa Mswada wa BBI umeondoa dhana kuwa Dkt Ruto anadhibiti idadi kubwa ya wabunge katika bunge la kitaifa. Hii ni dalili na ishara ya kuwa ushawishi wa Tangatanga unaadhoofika kadri uchaguzi mkuu unapakaribia,” Bw Kimunya akawaambia wanahabari Ijumaa katika majengo ya bunge.

Aliandamana na kiranja wa wengi Emmanuel Wagwe, naibu wake, Maoka Maore na kiranja wa wachache Junet Mohamed.Kando na Bw Ngunjiri, wabunge wa Tangatanga waliounga mswada huo pamoja na mahasidi wao wa mrengo wa Kieleweke ni; Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Feisal Bader (Msambweni), David Ole Sankok (mbunge maalum), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Kubai Iringo (Igembe ya Kati), Malulu Injendi (Malava), Purity Kathambi (Njoro), Martha Wangari (Gilgil), miongoni mwa wengine.

Jana, migawanyiko iliendelea kushamiri miongoni mwa wabunge wa wabunge wa mrengo huo kuhusu jinsi walipigia kura Mswada wa BBI.Bi Wangari alitofautiana na mwenzake wa Mathira Rigathi Gachagua katika hafla ya mazishi huku Gachagua akidai wabunge walihongwa ili kuunga mkono mswada huo.

Mbunge huyo wa Gigil alisema alipiga kura ya “NDIO” kwa Mswada wa BBI kutokana na manufaa yake, haswa ugavi wa rasimali katika kaunti ambapo asilimia 35 ya mapato yatagatuliwa ukipitishwa katika kura ya maamuzi.

You can share this post!

Wapwani kukosa maji huku miradi ya Sh70b ikikwama

Huyu Fofana “The Rock” apigiwa mahesabu na Man-United