• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Wavulana wang’aa idadi ya wasichana ikiongezeka

Wavulana wang’aa idadi ya wasichana ikiongezeka

Na CHARLES WASONGA

WAVULANA waling’aa ikilinganishwa na wasichana katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa 2020 yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu, George Magoha.

Hii ni licha ya kwamba, tofauti kati ya idadi ya watahiniwa wa kike waliofanya mtihani huo ilipungua kwani kati ya jumla ya wanafunzi 747,161, 366,834 walikuwa wasichana huku wavulana wakiwa 380,327Miaka iliyotangulia, wasichana walikuwa wakiwatoa jasho wavulana kwenye mtihani huo.

Katika orodha ya watahiniwa 15 bora kwenye mtihani wa mwaka jana, kulikuwa na wavulana wanane, wakiongozwa na Simiyu Robin Wanjala kutoka Shule ya Upili ya Murang’a.

Alipata gredi ya A yenye alama ya wastani ya 87.3. Alifuatwa na Allan Wasonga Udoma wa Shule ya Upili ya Agoro Sare (Homa Bay) na Sharon Chepng’etich Terer wa Shule ya Upili ya Kenya High, waliopata alama 87.173 kila mmoja.

Wavulana wengine katika orodha hiyo ni; Maraisi Bob Ongare (Shule ya Upili ya Alliance, 87.139, Kipkoech Mark Kogo (Shule ya Upili ya Alliance, 86.106), Kenneth Oranga (Shule ya Upili ya Kapsabet, 87.049), Henry Madaga (Shule ya Maranda, 87.046), Pile Ron George (Shule ya Upili ya Kapsabet, 86.970) na Kiprono Howard (Maranda, 86.949).

Mbali na Sharon Ng’etich, wasichana wengine walioorodheshwa miongoni mwa 15 bora ni; Esther Mbugua (Kenya High, 87,113), Patience Chepkorir (Kenya High, 87.046), Musomba Edith (Shule ya Upili ya Wasichana ya Machakos, 87.013), Lesly Loice Wanjiku (Kenya High), Jelimo Debra (Kenya High, 86.947) na Buluma Daisy Nerime (Kenya High).

Aidha, kaunti 15 zilisajili idadi ya juu ya wasichana kuliko wavulana katika mtihani huo wa KCSE ikilinganishwa na kaunti 17 katika mtihani huo mwaka wa 2019.

Kaunti hizo 15 ni; Taita Taveta, Kwale, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Machakos, Kitui, Meru, Nandi, Elgeyo Marakwet, Kakamega, Vihiga na Kisumu.

You can share this post!

Tetesi kuhusu ukosefu wa sodo shuleni ni uongo mtupu –...

Wanafunzi 604, 031 kujiunga na mafunzo ya kiufundi