• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Madiwani 78 wakataa mwaliko wa kukutana na Moi

Madiwani 78 wakataa mwaliko wa kukutana na Moi

Na FRANCIS MUREITHI

SIASA za ubabe kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi zilichangia kutibuka kwa mkutano ambao mwenyekiti huyo wa Kanu alipanga na madiwani nyumbani kwake Kabarak wikendi iliyopita.

Licha ya mwaliko kutumwa kwa madiwani 78 wa Nakuru, mkutano huo ulifutiliwa mbali dakika za mwisho huku duru zikiarifu kuwa Bw Moi alinuia kuutumia kupigia debe azima yake ya urais na pia mswada wa BBI.

Tangu achaguliwe kama Seneta tangu mnamo 2013, Bw Moi hajawahi kuandaa mkutano wowote na madiwani wa Nakuru ambao wengi wao walichaguliwa kupitia tiketi ya Jubilee.

Imebainika kwamba wengi wa madiwani wanamuunga mkono Naibu Rais Dkt William Ruto na waliwashawishi wenzao wasihudhurie mkutano uliofaa kuandaliwa Kabarak.

“Hatukuelezwa ajenda ya mkutano huo lakini tulishuku unahusiana na siasa za 2022 na kwa kuwa madiwani wengi wapo nyuma ya Naibu Rais kisiasa, waliamua kutohudhuria mkutano huo,’ akasema diwani moja mwandani wa Dkt Ruto ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

Diwani mwengine ambaye pia anaunga mkono azma ya Dkt Ruto alifichua kuwa badala yake, waliandaa mkutano mbadala mjini Nakuru ambapo walijadili namna ya kuvumisha azima ya urais ya Dkt Ruto.

Bw Moi na Dkt Ruto wamekuwa wakishiriki siasa za ubabe katika eneo la Bonde la Ufa hasa kuhusiana na siasa za 2022 na mpango wa maridhiano (BBI).

You can share this post!

Historia matokeo yakitua siku 3 baada ya usahihishaji

Bandari: Wachukuzi watoa masharti kwa serikali