• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Hakimu atoa uamuzi wake kwa Kiswahili sanifu

Hakimu atoa uamuzi wake kwa Kiswahili sanifu

Na BRIAN OCHARO

HAKIMU wa Mahakama wa Shanzu, Mombasa ameweka historia mpya kwa kutoa uamuzi wa kesi kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Ni desturi ya mahakama za hapa nchini kwa majaji na mahakimu kuandika kesi zao kwa kutumia Kiingereza lakini Hakimu Mwandimizi Mkuu David Odhiambo ameweka rekodi mpya wakati wa kesi ya mtu aliyeshtakiwa kwa shtaka la unajisi.

Katika kesi hiyo, Bw Kai Hanjari Murira alishtakiwa kwa kosa la kujaribu kunajisi mtoto mwenye umri wa miaka 14.

Baada ya kusikiza pande zote mbili, Hakimu Odhiambo alibaini kuwa mshukiwa ndiye aliingia kwa chumba cha mlalamishi kwa nia ya kumnajisi.

Bw Odhiambo alianza kutoa hukumu yake kwa kutaja wimbo wa ‘Kadzora’ wa mwimbaji mashuhuri wa mtindo wa Bango Mzee Ngala, unaoeleza juu ya utamu wa Kadzora ambayo ni kitoweo cha nyama ya panya inayoliwa kwa baadhi ya jamii za Pwani.

Ijapokuwa mnyama huyo ni kitoweo kwa baadhi ya jamii, kwa upande mwingine huwa ni kero kwa jamii nyingine kwa kuharibu mimea. Hakimu huyo alitumia simulizi hilo kueleza kuwa hata kama kitu kinaoenakana kuwa kitamu, haimaanishi kinafaa kuliwa.

“Vile vile maishani kuna vyakula ambavyo huonekana vitamu lakini punde tu tunavyoala vinaleta madhara aidha kwa sababu hatufai kuvila ama ni vya wenyewe na havijaiva,” alisema Bw Odhiambo.

Mahakama iliiambiwa kuwa kisa hicho kilitokea mnamo Aprili 5, 2019, akiwa maeneo ya Kijiweni, katika kaunti ndogo ya Bamburi.

Mshukiwa anakabiliwa na shtaka mbadala ya kufanya kitendo kisichofaa na mtoto mdogo kinyume cha Sehemu ya 11(1) ya Sheria ya Ngono.

Bw Munira hata hivyo alikanusha mashtaka dhidi yake alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza miaka miwili iliyopita.

You can share this post!

PSG watinga fainali ya French Cup baada ya kudengua...

Mvua yazua mafuriko na yaletea wakazi hasara