• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
CHARLES WASONGA: Serikali inakosea kuwaongezea raia maskini ushuru

CHARLES WASONGA: Serikali inakosea kuwaongezea raia maskini ushuru

Na CHARLES WASONGA

MNAMO Julai 1, 2021 Wakenya wataanza kuonja athari za masharti ambayo Shirika la Fedha Ulimwengu (IMF) lilitoa kabla ya kuidhinisha mkopo wa Sh257 bilioni kwa Kenya mnamo Februari.

Mojawapo ya masharti hayo ni kwamba serikali iimarishe kiwango cha mapato yake, kutoka humu nchini, ili kupunguza mwenendo wa kukopa ili kuziba pengo katika bajeti yake.

Serikali imeanza kutii agizo hilo kwa kupendekeza nyongeza za aina mbalimbali za ushuru katika Mswada wa Fedha, 2O21 uliowasilishwa bungeni Ijumaa wiki jana.Lakini inasikitisha kuwa badala ya Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani kupendekeza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa na huduma ambazo hutumiwa na matajiri, amelenga bidhaa zinazotumiwa na raia wenye mapato ya chini.

Kwa mfano, Waziri anapendekeza kuwa mkate utozwe ushuru wa ziada ya thamani (VAT) wa asilimia 16. Hii ina baada kuwa ikiwa wabunge watapitisha mswada huo bila kuufanyia marekebisho, bei ya mkate wa kawaida (wa uzani wa gramu 400) utapanda kwa Sh6 kutoka Sh50 hadi Sh56 kuanzia Julai 1, mwaka huu.

Vilevile, bei ya pikipiki zinazotumiwa katika uchukuzi wa abiria, maarufu kama bodaboda, zenye thamani ya Sh100,000 kwenda juu, itaongezeka baada ya serikali kupendekeza zitozwe ushuru wa kiwango cha asilimia 15.

Isitoshe, wanaoendesha biashara mitandaoni, wengi wao wakiwa vijana, wataathirika kwa sababu watahitajika kulipa ushuru wa VAT wa kiwango cha asilimia 16.

Mapendekezo kama haya bila shaka yatawaumiza wananchi wa kawaida hasa wakati kama huu ambapo wengi wao wameathirika na makali ya janga la Covid-19.Hii ni licha ya kwamba yanalenga kuiwezesha serikali kuimarisha kiwango cha mapato yake ili kuiwezesha kufadhili bajeti ya kima cha Sh3.6 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 unaoanza Julai.

Ninadhani badala ya serikali kulenga bidhaa zinazotumiwa na mwananchi mnyonge kifedha, kama vile mkate, ingeongeza ushuru kwa bidhaa ambazo hutumiwa na tabaka la matajiri kama vile magari ya kifahari ya V8.

Pili, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) inafaa kuimarisha juhudi zake za kuwaandama matajiri ambao hukwepa kulipa ushuru wa kima cha mabilioni ya fedha.

Watu kama hawa, wengi wao wakiwa na ushawishi serikalini, ndio hukosesha serikali mapato kila mwaka.Kwa mfano, mnamo 2019 mmiliki wa kampuni ya kutengeneza mvinyo kwa jina African Spirit Ltd, Bw Hampfrey Kariuki alishtakiwa kwa kosa la kukwepa kulipa ushuru wa kima cha Sh41 bilioni.

Mwaka huo huo, mwasisi wa kampuni ya kutengeneza pombe ya Keroche Breweries alisukumwa mahakamani kwa tuhuma za kuhepa kulipa ushuru wa 14 bilioni. Kesi hizo zingali zinaendelea.

Ninaamini kuna mabwanyenye wengi nchini ambao hukwepa ushuru wa mabilioni ya fedha. Hawa ndio watu ambao KRA inapaswa kuwaandama badala ya kuwaongezea Wakenya masikini mzigo wa ushuru.

You can share this post!

Waibuka wa kwanza Nyeri licha ya kuwa ni zeruzeru

KCSE: Tana River yachechemea