• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:16 AM
Mwaura apoteza useneta rasmi na kiti kutangazwa wazi

Mwaura apoteza useneta rasmi na kiti kutangazwa wazi

Na CHARLES WASONGA

SASA ni rasmi kwamba Seneta Maalum Isaac Mwaura amepoteza wadhifa wake baada ya Spika wa Seneti Kenneth Lusaka kutangaza kiti hicho kuwa wazi.Hii ni baada ya chama cha Jubilee kumfurusha kwa tuhuma za kukaidi sera na misimamo ya chama hicho na kuwapigia debe wagombeaji wa vyama tofauti vya kisiasa katika chaguzi ndogo zilizopita.

“Umma unajulishwa kwamba kulingana na kipengele cha 103 cha Katiba na sehemu 37 ya Sheria ya Uchaguzi, wadhifa wa Seneta Isaac Mwaura ulisalia wazi kuanzia Mei 7, 2021,” Bw Lusaka alisema katika notisi iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali.

Tangazo la Spika huyo wa Seneti lilijiri baada ya Jopo la kutatua mizozo ndani ya vyama vya kisiasa (PPDT) wiki jana kuidhinisha hatua ya Jubilee kumfurusha Bw Mwaura.

Maalum

Mwanasiasa huyo ni miongoni mwa maseneta maalum sita wa Jubilee ambao walifukuzwa mnamo Machi mwaka jana kwa kutotii mwaliko wa kutakiwa kuhudhuria mkutano wa maseneta wa Jubilee uliongozwa Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.Wengine walikuwa Millicent Omanga, Naomi Jilo Waqo, Mary Seneta Yiane, Victor Prengei na Iman Falhada Dekow.

Hata hivyo, masaibu ya Bw Mwaura yaliongezeka baada ya PPDT kuamua kuwa chama cha Jubilee kilifuata sheria na taratibu zifaazo kumfurusha.

Lakini jopo hilo linaloongozwa na Desma Nungo, liliwaokoa wenzake watano kwa kuamua kuwa kufurushwa kwao kulitekelezwa kinyume cha sheria.Bw Mwaura aliteuliwa na Jubilee kuwa Seneta Maalum baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 ili awakilishe watu wanaoishi na ulemavu nchini.

You can share this post!

KCSE: Tana River yachechemea

Genge laibuka upya nakujeruhi watu 7 mtaani