• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Supkem yakana mgawanyiko kuhusu Idd

Supkem yakana mgawanyiko kuhusu Idd

Na WACHIRA MWANGI

VIONGOZI wa Kiislamu wamepuuzilia mbali ripoti kwamba, kuna tofauti miongoni mwa waumini kuhusu siku ya kukamilisha Ramadhan.

Kulingana na kaimu mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waisilamu nchini (Supkem), Hassan Ole Naado, tofauti katika kumaliza Ramadhan kati ya Waislamu hutegemea kuonekana kwa mwezi.

“Hii ni desturi na mila ya Kiislamu, hakuna chochote kibaya; hili ni suala la sharia. Kuna baadhi ya Waislamu ambao hutegemea Uangalizi wa mwezi Ulimwenguni, wakati wengine hutegemea uangalizi wa mwezi wa mkoa /mitaa kuanza au kumaliza kufunga kwao,” alisema.“Ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anayejua kilicho sawa au cha makosa,” Bw Naado aliambia Taifa Leo kwa simu.

Alisema chochote kinachofanyika kwa maarifa na nia njema kila wakati kitavutia baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Waislamu hawahitaji kuwa na wasiwasi kuhusu tofauti ya tarehe.

Bw Naado alitupilia mbali ripoti kuwa wale waliofungua Alhamisi walikiuka ushauri wa Kadhi Mkuu. “Kadhi Mkuu anatoa ushauri tu na mpokeaji ndiye atakayeamua ikiwa atachukua au kupuuza ushauri huo. Imejikita kabisa katika historia ya Kiislamu, ” aliongezea.

Alisisitiza kuwa tofauti katika kumalizika au kuanza kwa mwezi wa kufunga ni suala ambalo linashuhudiwa ulimwenguni kote bali si Kenya pekee.

Usiku wa Jumatano, Kadhi Mkuu Muhdhar akiwa Mombasa alitangaza siku rasmi ya sherehe za Eid kuwa Ijumaa.

“Tumeshauriana lakini hatujaweza kuuona mwezi leo nchini Kenya, Tanzania wala Zanzibar. Tumesikia habari hizo kuwa mwezi umeonekana lakini hatuwezi kuthibitisha habari hizo. Tunatangaza kuwa tutakamilisha siku 30 za kufunga mnamo Mei 13, ‘Kadhi Mkuu alisema wakati alitangaza kuwa Ijumaa ni siku ya kusherehekea siku kuu ya Iddi ya mwaka huu.

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho alisema kuwa, swala hilo halifai kuwa mjadala baina ya Waislamu.

“La muhimu zaidi ni kudumisha heshima. Jambo la siku gani Waislamu wanafaa kufungua au kufunga halipaswi kuwa hoja. Kila mtu asheherekee ile siku ameridhika nayo kuwa anafaa kufungua kulingana na kuonekana kwa mwezi. Sisi bado ni mandugu na jamii moja. Tusigawanyike,” Joho alisema.

Alisema mwezi wa Ramadhan umekuwa siku 30 za tafakari na kuwa watu wawe waangalifu wakisheherekea na kudumisha itifaki za Covid-19 ili kujiweka salama.

“Eid ni wakati wa kutoa. Lakini tuhakikishe tumeheshimu masharti yaliyowekwa kudhibiti ugonjwa wa Corona ili tuokoe maisha ya wenzetu. Hii ni siku ya msamaha, ukarimu na fadhila. Tuombeane na pia tusisahau kuiombea nchi yetu,” Gavana Joho alisema.

Wanasiasa wa Mombasa, wafanyabiashara, Maimamu na mashehe wametoa wito kwa Waislamu kupeana chakula kwa wasiojiweza kwani wengine wao wameumizwa kiuchumi na janga la Covid-19.

Mfanyabiashara wa Mombasa, Suleiman Shahbal aliwahimiza Waislamu kuendelea na masomo ya kutoa dhabihu wakati wa Ramadhan.

Amewataka waendelee kuwapa wasiojiweza hasa wale walioathiriwa kwa kupoteza kazi kutokana na janga hiloKamishna wa Kaunti ya Makueni ambaye alikuwa amehudhuria maombi katika msikiti wa Al Farouq alimshukuru Mungu kwa kuwezesha Waislamu kumaliza mfungo bila shida yoyote.

You can share this post!

DPP aagizwa kufichua ushahidi wa kesi ya ufisadi dhidi ya...

BENSON MATHEKA: Serikali iweke sera kulinda watoto wenye...