• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
BENSON MATHEKA: Serikali iweke sera kulinda watoto wenye mahitaji maalum

BENSON MATHEKA: Serikali iweke sera kulinda watoto wenye mahitaji maalum

Na BENSON MATHEKA

MATOKEO ya mwaka jana ya mitihani ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne KCSE yameonyesha kuwa watoto walio na mahitaji maalumu wanaweza kufanya vyema katika masomo wasipopuuzwa.

Baadhi ya watoto hao walipata alama bora katika mitihani hiyo licha ya kuwa na changamoto za kimaumbile na kukosa uwezo wa kuona.Kwa mfano, wanafunzi kadhaa kutoka shule ya upili ya Aquinas, jijini Nairobi walipata alama za A na B licha kuwa na matatizo ya kuona.

Wengine wa kutoka shule mbali mbali kote nchini pia walipata matokeo bora na kuwa miongoni watakaojiunga na vyuo vikuu nchini. Hii ni funzo kwa wazazi na jamii inayodharau na kupuuza watoto walio na ulemavu kwamba huwa wanakiuka haki za wanao wanapokosa kuwapeleka shule na kuwatelekeza.

Wanapotunzwa na kupatiwa nafasi ya kusoma, watoto hao wanaweza kuchangia pakubwa katika ujenzi wa taifa kama wengine wasio na changamoto za kimaumbile.

Kinachohitajika ni sera ya serikali kuhusu watoto hao ili watu wanaowatelekeza na kuwanyima haki yao wakiwemo wazazi wao wachukuliwe hatua kwa kukiuka haki zao.

La muhimu kabisa ni kuongeza idadi ya shule za watoto hao au kuweka mazingira yanayofaa katika shule na vyuo vikuu ili kuwawezesha kupata masomo bila kutatizika.

Wengi wao huwa wanakosa nafasi ya kusoma kwa sababu mazingira katika shule hayawafai.Kwa mfano, taasisi zote za elimu zinafaa kuwa na vifaa spesheli za watoto walio na ulemavu na walimu kupatiwa mafunzo ya kuwashughulikia.

Hii itahakikisha watoto wengi walio na changamoto za kimaumbile wanapata nafasi ya kufurahia masomo. Serikali pia inafaa kupanua shule za watoto walio na mahitaji maalumu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna moja katika kila kaunti ndogo.Sera ya elimu ya watoto walio na hali hii itahakikisha kwamba jamii inawaheshimu.

Hii itawaepusha na unyanyapaa ambao umefanya baadhi yao kukatiza masomo kwa kubaguliwa na wenzao katika shule za umma. Uwezo wao katika masomo umedhihirisha kwamba wakisaidiwa, wana uwezo mkubwa zaidi wa kujiendeleza na kujitengemea katika maisha.

Ni kweli kulea mtoto mwenye mahitaji maalumu sio jambo rahisi hasa kwa Wakenya masikini. Hata hivyo, kubuniwa kwa sera inayowahusu na jamii kuheshimu haki zao, wanaweza kusaidiwa kubadilisha maisha yao. Iwapo sera hiyo ipo, inafaa kutekelezwa kikamilifu.

You can share this post!

Supkem yakana mgawanyiko kuhusu Idd

CHARLES WASONGA: Elimu eneo la Kaskazini mwa Kenya...