• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
WANDERI KAMAU: Waliofanya KCSE wazingatie nidhamu kufaulu maishani

WANDERI KAMAU: Waliofanya KCSE wazingatie nidhamu kufaulu maishani

Na WANDERI KAMAU

N ILIPOMALIZA Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) zaidi ya miaka kumi iliyopita, nilihisi kama ningeibuka mwanafunzi bora zaidi nchini, baada ya matokeo hayo kutangazwa.

Hata hivyo, ndoto yangu haikutimia, ijapokuwa nilihitimu na kufaulu kujiunga na chuo kikuu. Kabla ya kwenda chuoni, moja ya mambo yaliyokuwa yakiwasumbua sana watahiniwa wenzangu ni kuhusu kozi ambazo wangechagua ili “kutosumbuka kutafuta kazi” pindi watakapomaliza masomo yao.

Kulikuwa na dhana eti taaluma za sayansi ndizo zilikuwa bora zaidi.Kuna wale walioshabikia kusomea sheria, udaktari na uhandisi. Miongoni mwa wanafunzi wengi, hizo ndizo “taaluma bora zaidi.”

Kwa kuwa shule nilikosomea ilikuwa miongoni mwa zile zilifaulu sana mwaka huo, wanafunzi wengi walifanikiwa kwenda vyuoni kusomea taaluma nilizotaja awali.Hata hivyo, kile ambacho kiliniatua moyo, hadi sasa, ni kuwa baadhi yao hawakupata mafanikio maishani kama walivyokusudia.

Baadhi walifukuzwa vyuoni kwa utovu wa nidhamu, wengine wakajiingiza kwenye utumizi na ulanguzi wa mihadarati, huku wengine wakiziacha kozi zao baada ya kuwalemea.Kilichonishtua ni kuwa baadhi ya wale waliojikuta kwenye maovu hayo ni wanafunzi waliopata alama bora sana kwenye mtihani wao.

Waliogopwa na wanafunzi wengi, hasa waliokuwa hawafanyi vizuri sana masomoni, kwani walichukuliwa kama “masogora wasioshindwa.”

Lengo kuu la kumbukumbu hii ni kutoa ujumbe kwa wanafunzi waliopata matokeo ya KCSE wiki hii: Nidhamu ndiyo itakayowawezesha kutimiza ndoto zao popote waendako.

Kumekuwa na malalamishi mengi kuwa licha ya kizazi cha sasa kuwa na wanafunzi werevu na wenye uwezo mkubwa kimasomo, wengi hao hawana uvumilivu maishani.Ingawa hilo limekuwa likihusishwa na mazingira wanayolelewa, ni wakati wafahamu hawatakuwa chini ya uangalizi wa wazazi wao daima.

Katika vyuo vikuu ama vyuo anuwai, wazazi wao hawatakuwepo kufuatilia nyendo zao. Hawatakuwepo kuwaambia wahudhurie masomo yao au la. Hawatakuwa karibu nao kuwaamulia aina ya marafiki watakaochagua kutangamana nao.

Huo utakuwa uamuzi wao wenyewe.Pengine kile wazazi wao watawasaidia nalo ni kuwapa mwongozo tu, bali si kufuatilia mienendo yao kila siku.

Ni muhimu kwao kufahamu kuwa katika mazingira yenye uhuru mwingi kama vyuo vikuu, watakuwa na nafasi ya kujenga ama kuvuruga misingi ya maisha yao.Huu ni wakati wao kufahamu hii ni nafasi pekee walio nayo kuamua mwelekeo na hatima ya maisha yao.

Ni nafasi pia ya wazazi kutangamana kwa undani na wanao kuhakikisha hawatatekwa na maovu watakapojiunga na vyuo.

[email protected]

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Suluhu itafutwe kwa vita kati ya Israeli na...

Uamuzi wa mahakama wavuruga urithi wa Uhuru 2022