Wakenya wafurahia Mahakama Kuu kuzima densi ya Reggae

Na MARY WANGARI

WAKENYA jana walifurika katika mitandao ya kijamii kuelezea maoni mseto kufuatia Uamuzi wa Mahakama Kuu uliofutilia mbali Mpango wa Maridhiano (BBI) Alhamisi.

Jopo la majaji Bi Teresia Matheka, mabwana Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah na Chacha Mwita liligeuka kipenzi kwa wananchi baada ya kutupilia mbali mchakato wote kuhusu mswada wa BBI kwa misingi ya ukiukaji sheria Kupitia heshitegi #BBIJudgement, viongozi na wananchi kwa jumla walijitosa mitandaoni kueleza hisia zao, baadhi wakiunga mkono uamuzi huo huku wengine wakiupinga.

Naibu Rais William Ruto anayeongoza kambi ya Tangatanga ambayo imekuwa mstari wa mbele kupinga BBI hakuweza kuzuia furaha yake.

“Kuna Mungu mbinguni anayeipenda Kenya mno. Jina la Mungu lisifiwe milele,” alisema Dkt Ruto. “Uamuzi wa leo ni thibitisho tosha kuhusu katiba na utawala wa sheria,” alisema kiongozi wa Narck Kenya Martha Karua.

“Wakati historia ya Kenya itakapoandikwa ipasavyo, mchango wa Majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Chacha Mwita na Teresia Matheka utaandikwa kwa herufi za dhahabu. Ni miongoni mwa manabii wachache Wakenya waliosalia ambao hawajainamia Baali,” alisema Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

“Ni mpaka lini nitaendelea kuwaambia Wakenya kuwa tuna serikali hasimu, Mwanasheria Mkuu asiyefaa na Bunge lililonyamazishwa. Tulihitaji kweli kwenda kortini kutatua maswali hayo ya kimsingi kuhusu mswada wa BBI,”alihoji wakili Nelson Havi.

Hata hivyo, kunao waliokosoa uamuzi huo wakikosoa Idara ya Mahakama kwa kuwa na kisasi na kuwalaumu washauri wa Rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki.

“Natarajia kujiuzulu kwa watu waliompotosha Rais wakiongozwa na Bw Kihara. Kwa sababu ya dosari kisheria na kikatiba katika mchakato wa BBI baadhi yetu tulijua BBI ingeambulia patupu. Ulikuwa mchakato wa kisiasa,” alihoji Eddie Mugo.

“Upuzi wa Idara ya Mahakama huzaa hali hatari. Vipengele vya kudumu ni upuzi tu wa kikatiba. Ni kipindi hatari tu kinachoweza kubadilisha hali hiyo. Wakenya wasioelewa mambo wasijishughulishe na ujumbe huu lakini mmeonywa,” alisema mchanganuzi wa sheria Mutahi Ngunyi.

Habari zinazohusiana na hii

MAYATIMA WA BBI