• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Mzee aliyerushwa nje ya SGR apatikana hai siku 4 baadaye

Mzee aliyerushwa nje ya SGR apatikana hai siku 4 baadaye

Na PAUL WAFULA

MZEE aliyerushwa nje ya gari moshi kwenye reli ya kisasa (SGR) Jumanne iliyopita alipatikana akiwa hai jana baada ya kukaa siku nne kwenye baridi.

Familia ya Bw Peterson Mwangi Ngunyi, ilisema jana kuwa mzee huyo alipatikana akiwa na njaa, bila viatu, mchovu lakini akiwa hai. Alipatikana eneo la Buru Buru Phase 1 huku akionekana mgonjwa bila viatu wala koti.

Masaibu ya Mzee huyo yalianza mnamo Mei 11, 2021, alipoabiri treni ya abiria ya SGR akielekea Mombasa.Mwanamume huyo mkongwe, ambaye ana matatizo ya akili, aliabiri Madaraka Express ya saa mbili asubuhi, kuelekea pwani kutoka kituo cha Nairobi eneo la Syokimau.

Alirushwa nje katika kituo cha Athi River kwa misingi kuwa hakuwa na tiketi inayofaa.Familia yake hata hivyo, imewasilisha rekodi za tiketi iliyonunuliwa na kusema kuwa Bw Mwangi ana usahaulivu wa kiwango cha chini ambao hauathiri shughuli zake za kimaisha.

Walisema kuwa Bw Mwangi aliporushwa nje, walijulishwa kwamba alikuwa na tiketi ya mtoto ilhali maelezo katika ujumbe waliopokea baada ya kulipa kwa kutumia M-pesa , yanadhihirisha ilikuwa tiketi ya mtu mzima, Second Class, Coach 5 Seat 61, Train N2.

Familia hiyo ilishangaa vilevile ni kwa nini wahudumu wa treni hiyo hawakuwa na utu na kujali kile ambacho kingemtendekea mzee kama huyo kabla ya kumrusha nje katikati ya safari yake.

Kenya Railways ikijitetea, inasisitiza kuwa wakati wa kukagua tiketi kwenye treni, wahudumu wake waligundua Bw Mwangi alikuwa na tiketi isiyofaa.

“Tiketi hiyo yenye utata ilikuwa ya abiria aliyekuwa amesafiri siku iliyotangulia kutoka Mombasa kuelekea Nairobi,” Kenya Railways ilisema kupitia taarifa.

Maafisa wa treni hiyo walimwagiza mzee huyo mwenye umri wa miaka 71 kuwapigia simu jamaa zake ili walipie safari yake lakini hakuwa na simu wala nambari yoyote ambayo angetumia kuitishia usaidizi baada ya kushinikizwa na maafisa hao, Bw Mwangi aliamua kushuka katika Kituo cha Athi River.

Kwa sababu alikuwa mgonjwa, hakujua pa kwenda na amekuwa hajulikani alipo kwa siku kadhaa.

You can share this post!

JAMVI: Mirindimo mipya ya Tangatanga baada ya BBI kuzikwa

DINI: Akili yako itawaliwe na mawazo mema usiwe adui wa...