• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Serikali yaonya dhidi ya fujo katika uchaguzi wa Bonchari

Serikali yaonya dhidi ya fujo katika uchaguzi wa Bonchari

Na WYCLIFFE NYABERI

MSHIRIKISHI wa serikali katika eneo la Nyanza Bw Magu Mutundika ameonya watakaozua fujo kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii kuwa watakabiliwa vilivyo.

Wakazi wa Bonchari wataelekea debeni Jumanne kumchagua mbunge wao mpya baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wao marehemu Oroo Oyioka aliyeaga dunia mwezi Februari.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilisema kwamba uchaguzi utafanyika ilivyopangwa licha ya Mahakama Kuu kusema haina idadi ya makamishna wanaohitajika.

Kufuatia kampeni zilizoshuhudia joto la kisiasa na wanasiasa kulaumiana miongoni mwao, sasa serikali imedokeza kuwa imepokea ripoti kwamba kuna watu wanaopanga ghasia kwenye uchaguzi huo.

Akiongea na wanahabari jana katika afisi za kamishna wa kaunti ya Kisii, Bw Mutindika alidokeza kuwa tayari wamepokea taarifa za ujasusi kuwa kuna magari mawili yanayozunguka Bonchari, yakiwa yamebeba silaha butu na mapanga yatakayotumiwa na wahuni kuleta fujo siku ya upigaji kura.

“Baadhi ya wahuni wanasemekana kutoka nje ya kaunti hii na wanataka kuzua fujo Jumanne. Kuweni na uhakika kwamba tumejipanga kwa hili na tutawakabili sana,” akasema Bw Mutundika.

Mshirikishi huyo aliongeza kwamba tayari wameyatambua majina ya watu wanaoaminika kuhusika kwenye upangaji wa ghasia na watakamatwa muda wowote.

Aidha, Bw Mutindika aliwaonya wanasiasa kuwa hawatasazwa ikiwa watapatikana kuhusika kwenye upangaji wa uovu wowote. Alimtaka kamanda wa polisi katika kaunti ya Kisii kuingilia kati na kuwakamata wale watakaopatikana wakipanga machafuko Bonchari.

Tayari watu watatu wamekamatwa na watafikishwa mahakamani.

Siku ya Ijumaa, mtu mmoja alipata majeraha mabaya ya panga kichwani na mkononi na wengine watatu wakaumizwa kwenye hafla moja ya mazishi iliyofanyika sehemu za Botoro baada ya wafuasi wa wapinzani tofauti kutofautiana.

Baada ya kampeni za uchaguzi huo kukamilika Jumamosi, Bw Mutindika aliongeza kuwa juhudi za kuwahonga wapiga kura zilikuwa zimeongezeka maradufu.

Alisema baadhi ya watu walikuwa wakizunguka na kununua vitambulisho vya wapiga kura huku wakijiandaa kwenye uchaguzi huo mradi wakitwae kiti hicho kwa njia zozote.

Bw Mutindika alisema tayari washukiwa wametiwa mbaroni na serikali itawashtaki ipasavyo.

“Hatutaki watu wa Bonchari wanyimwe haki yao ya kumchagua mbunge wao. Tunawaomba wanasiasa wasijihusishe kwa hili kwani wataishi kujutia,” akasema Bw Mutindika.

Akizungumzia swala la maafisa wa polisi kuvamia boma la gavana wa Kisii Bw James Ongwae Alhamisi usiku na kuwafukuza wanasiasa waliokuwa naye, Bw Mutindika alisema kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i hakuhusika kwa vyovyote katika tukio hilo na hivyo basi wale wanaomlaumu wanafaa kukoma mara moja.

“Huo haukuwa mwaliko wa kawaida wa kula chakula cha jioni. Tunalifahamu hilo vyema na polisi wanafanya kazi yao ya kawaida ya kutuliza hali.”

“Hatumpendelei mtu yeyote. Kila mtu anaweza kuandaa chakula cha jioni lakini wao walikuwa wamepanga mkutano,” akasema mshirikishi huyo kuwajibu viongozi wa ODM waliodai walikuwa wamealikwa kwenye chajio.

Bw Mutindika alimtaka gavana Ongwae kutohusisha jina la Dkt Matiang’i kwenye masahibu yake.

Uchaguzi mdogo wa Bonchari umewavutia wawaniaji 13. Tatu kati yao ni wanawake na siasa hizo zitashuhudia vyama vikuu nchini kumenyana kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wao ni: Jonah Onkendi Ondieki ( The New Democrats), Mary Sally Otara (United Green Movement), Beatrice Nyabuto ( Maendeleo Chap Chap) ,Eric Oigo (National Reconstruction Alliance), David Ogega ( Kenya Social Congress).

Wengine ni Zebedeo Opore (Jubilee), Teresa Bitutu (United Democratic Alliance), Pavel Oimeke (ODM), Kelvin Mosomi (Party of Democracy Unity), Jeremiah Matagaro (Agano Party), Charles Mogaka ( Progressive Party of Kenya), Paul Matagaro, ( Mwangaza Party) na Victor Omanwa ( Party of Economic Democracy)

You can share this post!

Uhuru apangiwa kuzuru Pwani baada ya Raila

Uvundo tele Nairobi huku NMS ikizembea