Usalama waimarishwa Juja tayari kwa uchaguzi mdogo Jumanne

Na LAWRENCE ONGARO

UCHAGUZI mdogo wa kiti cha ubunge Juja utafanyika Jumanne, Mei 18, 2021, na tayari wapigakura wamehimizwa watawanyike baada ya kukamilisha kupiga kura.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyanga, alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia kuenea kwa homa ya Covid-19.

“Tunawashauri wapigakura wafuate sheria, masharti na kanuzi za Wizara ya Afya kusaidia katika kupunguza kusambaa kwa corona. Vile vile hatutaki kuwe na fujo kati ya walinda usalama na wapigakura,” alifafanua Bw Wanyanga.

Alisema kutakuwepo vituo vya kupiga kura 184 ambapo kila sehemu itakuwa na ulinzi wa kutosha.

Alisema baada ya kupiga kura kila mmoja ameshauriwa kurudi kwake nyumbani ili kusubiri matokeo huko.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Kiambu, Bw Ali Nuno, alitoa onyo kali kwa vijana ambao “huenda pengine wamepanga kuzua vurugu katika vituo vya kura.”

Alisema yeyote anayepanga kuzua vurugu atakabiliwa na sheria kikamilifu.

Alieleza kuwa kutakuwa na walinda usalama wa kutosha na kwa hivyo “wale wanaopanga kuleta shida watajilaumu wenyewe.”

Afisa huyo wa usalama aliwashauri wawaniaji kiti hicho cha ubunge wawajulishe maajenti wao jinsi ya kulinda kura zao ili wasilete malalamiko baadaye.

Kiti hicho cha Juja kiliachwa wazi baada ya mbunge Francis ‘Wakapee’ Waititu kufariki baada ya kuugua saratani ya ubongo kwa zaidi ya miaka miwili.

Kiti hicho kinagombaniwa na wawaniaji 10 akiwemo mkewe marehemu Bi Susan Njeri Waititu wa chama cha Jubilee.

Wengine ni Bw George Koimburi (People Empowerment Party), Dkt Joseph Gichui (mgombea wa kujitegemea), James Marungu Kariuki (mgombea wa kujitegemea), Kariuki Ireri (mgombea wa kujitegemea), Kenneth Gachuma (National Liberal Party), Anthony Kirori (Maendeleo Chap Chap) na Muiga Rugara (mgombea wa kujitegemea).

Afisa mkuu wa uchaguzi eneo la Juja Bw Justus Mbithi, alisema tayari mipango yote imekamilika huku wakitarajia uchaguzi utakuwa wa amani.

Alisema kila mpigakura kituoni atapimwa joto la mwili huku pia akilazimika kunawa mikono kabla ya kupiga kura ili kuzuia maambukizi ya Covid-19.