• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
WARUI: Elimu: Serikali itambue mchango wa shule za kibinafsi

WARUI: Elimu: Serikali itambue mchango wa shule za kibinafsi

Na WANTO WARUI

MATOKEO ya mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne, KCSE yaliyotangazwa juma lililopita yalizua hisia mbalimbali kwa watu tofauti.

Mojawapo ya hisia hizo ni kama mtihani huo ulisahihishwa vizuri kutokana na sababu kwamba matokeo yalitolewa siku chache tu baada ya usahihishaji kukamilika.

Hata hivyo, Wakenya wengi hasa jamaa za wanafunzi waliofanya vyema hawakutaka kujua zaidi ila kusherehekea ushindi wa watoto wao.

Hili ni jambo la kawaida kila mwaka baada ya serikali kutangaza matokeo. Licha ya wanafunzi kusherehekea ushindi wao, shule ambazo huwa zimewatoa washindi pia haziachwi nyuma katika sherehe na mbwembwe hizi.

Kinyume na ilivyo katika matokeo ya darasa la nane ambako shule nyingi zinazochukua nafasi za juu ni zile za kibinafsi, katika shule za sekondari ni shule za umma huchukua nafasi hizo bora.

Kwa mfano katika matokeo ya mwaka uliopita wa 2020, shule zilizonyakua nafasi za juu ni Shule ya Wavulana ya Kapsabet, Kenya High, Shule ya Mang’u , Shule ya Alliance miongoni mwa nyingine.

Lakini kando na shule hizi, kuna shule za kibinafsi nyingi ambazo zilitoa matokeo mazuri sana. Kuna shule kama vile Strathmore, Moi Kabarak, Anestar Nakuru na Light Academy miongoni mwa nyingine nyingi.

Shule hizi za kibinafsi zimeonyesha kuwa zinalenga kuimarisha na kuchangia katika elimu humu nchini.

Kutokana na mifano kama hii na idadi kubwa ya shule za kibinafsi nchini, ni dhahiri kuwa shule za kibinafsi; zile za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu ni mshirika mkuu wa elimu nchini na serikali haina budi kukubali hivyo.

Mara kwa mara baadhi ya maafisa wakuu katika wizara ya elimu wamesikika wakikejeli shule hizi kana kwamba zipo kinyume cha sheria. Idadi kubwa iliyoko nchini ya wanafunzi haiwezi kutoshelezwa na shule za umma pekee.

Aidha, ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kusomea na walimu pia ni changamoto nyingine kwa serikali.

Kuwepo kwa shule za kibinafsi ni jambo halali ambalo serikali inastahili kukubali na kuungana mkono ili kuwapa wananchi wake elimu bora inayomfikia kila mmoja nchini.

Kama ilivyo katika sekta nyingine nchini ambako mchango wa watu binafsi unasaidia kuimarisha sekta hizo, kwa mfano utalii, basi hakuna kasoro katika sekta ya elimu na haifai kuonekana kana kwamba wasimamizi na wenye shule hizi wanavunja sheria wakitoa elimu kwa njia zifaazo.

Lazima itambulike kuwa kuwepo kwa shule za kibinafsi ni njia moja ya serikali katika kujiimarisha katika masuala ya elimu, ambayo hatimaye yatachangia pia kwa uchumi wa nchi.

You can share this post!

WANYAMA: BBI: Uamuzi wa korti waweza kukosolewa

DIMBA: Washasema Waswidi: Huyu Alex Isak ndiye Zlatan mpya