• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
DIMBA: Washasema Waswidi: Huyu Alex Isak ndiye Zlatan mpya

DIMBA: Washasema Waswidi: Huyu Alex Isak ndiye Zlatan mpya

Na GEOFFREY ANENE

SWALI nani atajaza nafasi ya mchana nyavu matata Zlatan Ibrahimovic atakapostaafu kabisa kuchezea Uswidi, linasalia kuwa kitendawili.

Hata hivyo, huenda jibu likatoka kwa kinda Alexander Isak.

Ingawa mwanya wa talanta kati ya Waswidi hawa wawili ni mkubwa sana, kwa umbali Isak amekuwa akionyesha dalili anaweza kujaribu kutegua kitendawili hicho baada ya kufana Real Sociedad msimu huu.

Bado Isak atalazimika kufanya kazi ya ziada kufikia Ibrahimovic – nyota wa zamani wa Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, Paris Saint-Germain na Manchester United – ambaye anaendelea kuvuma AC Milan akiwa na umri wa miaka 39.

Isak alizaliwa Septemba 21 mwaka 1999 mjini Solna, Uswidi.

Amepata jina la utani “The New Zlatan” kutokana na bidii aliyonayo ya kutafuta mabao; pia ni mrefu.

Kinda huyu k ana asili ya Afrika Mashariki. Wazazi wake kutoka Eritrea walihamia Uswidi wakati nchini hiyo inayopakana na Sudan, Ethiopia na Djibouti na Bahari ya Shamu ilikuwa haikaliki kutokana na ukosefu wa amani.

Mswidi huyo, ambaye anasemekana huzuru Eritrea mara kwa mara, alianza uchezaji wa soka akiwa na umri wa miaka sita katika klabu ya AIK ambayo imeajiri beki Mkenya Eric ‘Marcelo’ Ouma.

Isak alifanyiwa majaribio katika klabu hiyo na kuyapita. Alipenda majukumu ya ufungaji wa mabao alipofika miaka ya 13 akitumai kufuata nyayo za shujaa wake ambaye ni yule “muuaji” mmoja Ibrahimovic.

Akiwa na umri wa miaka 17, Isak alifanya uamuzi wa kijasiri wa kuacha familia yake nchini Uswidi na kuenda Ujerumani kuendeleza ukuaji wake wa soka.

Alikuwa ameonyesha talanta ya hali ya juu akiwa AIK kabla ya kujiunga na Borussia Dortmund inayopendwa na chipukizi kwa sababu ya kuwachezesha zaidi na kuwapa fursa ya kujiendeleza.

Hakupiga hatua kubwa Dortmund iliyompeleka nchini Uholanzi kwa mkopo katika klabu ya Willem II. Alipata kujinyanyua kutoka alikokuwa amepoteza mwelekeo na akanyakuliwa na Sociedad.

Msimu huu wa 2020-2021, Isak amejitokeza kuwa tegemeo wa Sociedad kiasi cha kuvutia “mashetani wekundu” wa Manchester United pamoja na Chelsea ya kocha Thomas Tuchel na Liverpool inayotiwa makali na Jurgen Klopp.

Ripoti zinasema kuwa Sociedad inajiandaa kufikisha Isak sokoni mwisho wa msimu huu.

Inaaminika kuwa katika kandarasi yake itakayokatika Juni 30, 2024, kuna kifungu kinachomruhusu kuondoka kwa Sh9.1 bilioni.

Kiasi hicho kitamfanya kuwa mchezaji aliyehama Sociedad kwa ada kubwa katika historia ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uhispania.

Tetesi zinadai kuwa miamba wa Uhispania Barcelona pia Real Madrid wako makini kutafuta huduma za Isak.

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich pia hawajawachwa nyuma kutamani kuwa na huduma mshambuliaji huyo.

Isak ametetemesha nyavu za wapinzani mara 30 katika michuano 83 ya kushindana tangu atue ugani Anoeta.

Karibu nusu ya idadi hiyo ya magoli amepata msimu huu wa 2020-2021. Kazi yake imeweka Sociedad pazuri kujikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Uropa. Kwa sasa, klabu yake inakamata nafasi ya tano kwenye ligi hiyo ya timu 20.

Kwa hivyo, si ajabu anapigiwa hesabu na makocha wengi. Kocha Ole Gunnar Solskjaer inasemekana anataka kumfanya Isak kuwa mrithi wa nafasi ya Edinson Cavani msimu ujao.

Naye Tuchel, ambaye alikuwa kocha wa Dortmund wakati Isak alijiunga nayo, ameridhishwa na kazi yake nchini Uhispania.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinaamini kuwa Isak anaweza kuwa sajili muhimu ugani Stamford Bridge kuchukua nafasi ya mshambuliaji Olivier Giroud ambaye miaka ya kustaafu imeanza kubisha hodi.

Pia, Isak anaweza kusaidia katika kuwa mshambuliaji mbadala wa Timo Werner ambaye hajafikia matarajio ya wengi tangu awasili kutoka Leipzig katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichopita.

Washambuliaji wa Liverpool, Roberto Firmino na Mohamed Salah wamehusishwa na uhamisho kwa hivyo huenda “the Reds” hawatafikiria mara mbili kuhusu kunyakua Isak, ingawa bei yake ya juu inaingiza kiwewe klabu zinazommezea mate.

Real Madrid ya kocha Zinedine Zidane, ambayo ilikataliwa na Isak kabla ajiunge na Dortmund, bado haijakufa matumaini.

Imeweka Isak kwenye rada yake isipofaulu kusaini makinda Erling Haaland (Borussia Dortmund) na Kylian Mbappe (Paris Saint-Germain).

Isak, ambaye alijiunga na Sociedad mnamo Julai 1 mwaka 2019 akitokea Wilhelm II nchini Uholanzi, amejumuishwa katika timu ya taifa ya watu wazima ya Uswidi mara 20 na kuifungia magoli sita.

Atategemewa kuongoza mashambulizi ya Uswidi kwenye Kombe la Bara Ulaya mnamo Juni 11 hadi Julai 11. Uswidi iko Kundi E pamoja na Uhispania, Poland na Slovakia.

Isak tayari amevuna Sh550.4 milioni kutokana na uchezaji wa soka. Anapokea mshahara wa Sh2.9 milioni kila wiki (Sh149.2 milioni kila mwaka) kambini mwa Sociedad.

You can share this post!

WARUI: Elimu: Serikali itambue mchango wa shule za kibinafsi

GUMZO: PSG tayari kutoa mabunda ili kumleta Mo’ Salah...