• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Usalama waimarishwa wapigakura wakitarajiwa kumchagua mbunge wa Bonchari

Usalama waimarishwa wapigakura wakitarajiwa kumchagua mbunge wa Bonchari

Na WYCLIFFE NYABERI

WAKAZI wa eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii wanaelekea debeni kesho Jumanne kumchagua mbunge wao mpya baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wao Oroo Oyioka.

Maandalizi yote ya uchaguzi huo mdogo yamekamilika na afisa wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika eneo hilo Bw Benson Ambuko amedokeza kuwa wanatarajia shughuli hiyo kuendeshwa kwa amani na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Eneobunge la Bonchari lina jumla ya wapigakura 52,955 kutoka wadi nne za Bomorenda, Riana, Bogiakumu na Bomariba.

Akiongea na wanahabari jana mjini Suneka baada ya kuongoza hafla ya kuzifungua karatasi za kupigia kura na vifaa vingine, Bw Ambuko alisema kuwa maafisa watakaosimamia uchaguzi huo wamepokea mafunzo ya kutosha kuhakikisha upigaji kura unaendeshwa vilivyo.

Aidha afisa huyo amehimiza wapigakura kujitokeza kwa wingi ili kutekeleza wajibu wao kikatiba wa kumchagua kiongozi atakaye wawakilisha bungeni.

“Tuko tayari kwa uchaguzi na kila kitu kimepangwa inavyostahili. Tunawaomba wapigakura wote wajitokeze kwa wingi,” Bw Ambuko akasema.

Kufuatia ujasusi wa serikali kwamba watu fulani walikuwa wakipanga kuzua fujo kwenye uchaguzi huo jinsi ilivyoshuhudiwa katika eneobunge la Matungu, hali ya usalama imeimarishwa.

Walinda usalama, kikiwemo kikosi cha GSU, wametumwa ili kuwapiga jeki wenzao wa polisi wa kawaida.

Mshirikishi wa serikali eneo la Nyanza Bw Magu Mutindika alitoa onyo kwa wahuni wasijaribu kuleta fujo katika uchaguzi huo.

Uchaguzi mdogo wa Bonchari umewavutia wawaniaji 13 ambapo watatu ni wanawake na vyama vikuu nchini vitamenyana kwenye kinyang’anyiro hicho.

 

Wao ni Jonah Onkendi Ondieki ( The New Democrats), Mary Sally Otara (United Green Movement), Beatrice Nyabuto ( Maendeleo Chap Chap), Eric Oigo (National Reconstruction Alliance), David Ogega ( Kenya Social Congress).

Wengine ni Zebedeo Opore (Jubilee), Teresa Bitutu (United Democratic Alliance), Pavel Oimeke (ODM), Kelvin Mosomi (Party of Democracy Unity), Jeremiah Matagaro (Agano Party), Charles Mogaka (Progressive Party of Kenya), Paul Matagaro (Mwangaza Party) na Victor Omanwa (Party of Economic Democracy).

You can share this post!

Demu aachwa kwa kukwamilia mzinga

Maandamano yaandaliwa Mombasa kulaani Israeli kwa mauaji ya...