• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
TAHARIRI: Mjadala wa bangi ufanywe kimakinifu

TAHARIRI: Mjadala wa bangi ufanywe kimakinifu

KITENGO CHA UHARIRI

MJADALA kuhusu kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi nchini unazidi kunoga, jaribio la hivi punde kisheria likitoka kwa waumini wa imani ya Rastafari (RSK).

Waumini hao jana waliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka matumizi ya mmea huo yahalalishwe wakisema unawasaidia wanapoabudu.

Miongoni mwa sababu walizotoa ni kuwa bangi ni dawa na ina nguvu za kiroho zinazowawezesha kuwasiliana na Mungu.

Kenya ilipiga marufuku matumizi ya bangi mnamo 1994 kupitia sheria ya kupambana na ulanguzi wa mihadarati na vileo, ambayo inajumuisha bangi kuwa miongoni mwa mihadarati.

Hata hivyo, bangi inatumika waziwazi mitaani kwa matajiri na vitongoji duni. Aidha, watu wamebuni njia za kuongeza ladha – na pengine thamani – kwa kuichanganya katika vitafunio kama vile biskuti, chokoleti, peremende na hata keki. Kwa njia hiyo pia wameweza kukwepa marufuku ya serikali.

Kwa sababu hiyo, mjadala kuhusu matumizi ya bangi unafaa kuzungumzia jinsi ya kudhibiti matumizi yake kwani tayari inatumika. Njia moja ni kuchukua mwelekeo uliotumika kudhibiti uvutaji sigara.

Bangi imethibitishwa na watafiti kuwa kiungo muhimu kutengeneza dawa ya kutuliza uchungu; muhimu sana katika kutibu magonjwa sugu kama kansa na maumivu mengine makali.

Kwa upande mwingine, madhara yake yamewafanya wengi kwenda kichaa kando na kudhoofika kimwili. Vijana wachanga wenye nguvu wameishia kuwa bwege na kumalizia pesa katika uraibu huu hatari.

Kwa kufuata mfano wa kampeni ya kudhibiti uvutaji sigara nchini, inawezekana kuondoa bangi vinywani mwa vijana na watu wengine waliosetwa na bidhaa hiyo.

Kuwe na hamasisho za wazi kuhusu madhara ya kiafya na kisaikolojia, ikiandamana na picha za kunata ili kuonyesha waraibu na waraibu wajao hatari wanayojitia ndani.

Pili, iwapo serikali itaruhusu kutengenezwa kwa bangi basi kutengwe sehemu maalum za kuvutia bangi ili wavutaji wasipate sababu ya kujificha nyumbani na maeneo ya sirini kufanya mambo yao.

Tatu, kuwe na mpangilio rasmi wa kuunda bangi ili kutathmini ubora wa bidhaa hiyo kama tu zingine. Kwa njia hiyo serikali pia itaweza kudhibiti mbinu za mauzo na hivyo kuzima njia za mkato.

You can share this post!

Tanzania: Kamati yapendekeza kuwepo kwa ‘lockdown’...

Waomba bangi ikubaliwe kufanyia ibada