• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Nakumbwa na hofu kuu ya kujifungua

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nakumbwa na hofu kuu ya kujifungua

Mpendwa Daktari,

Nina mimba ya miezi sita, na katika kipindi cha hivi majuzi nimekuwa nikikumbwa na hofu kuu kila ninapowazia kujifungua. Nilishuhudia hali ngumu nilipokuwa nikijifungua mtoto wangu wa kwanza, ambapo niliumwa sana tena kwa muda mrefu. Nitakabilianaje na hofu hii na napaswa kufanya nini mapema ili kuepuka uchungu kama ulionikumba wakati wa kwanza?

Amina, Mombasa

Mpendwa Amina,

Unayoshuhudia wakati wa ujauzito na uchungu wa uzazi huwa tofauti kutoka mimba moja hadi nyingine, na mara nyingi matukio hayo hayatabiriki kwa urahisi. Ni wanawake wachache sana hushuhudia kipindi kifupi cha uchungu wa uzazi na maumivu kiasi, wengi hukumbwa na maumivu makali kwa kipindi kirefu.

Tafadhali zungumza na daktari anayekushughulikia wakati wa ujauzito, au tafuta ushauri kutoka kwa mwanajinakolojia. Jadili wasiwasi wako na umweleze kuhusu ulichokumbana nacho wakati wa kwanza ili muunde mpango wa kujifungua.

Ikiwezekana, mnaweza panga mapema ili upewe dawa za kudhibiti uchungu wakati wa kujifungua. Ikiwa hali hii inachochewa wasiwasi mwingi, kwa mwongozo wa daktari unaweza pia chagua kufanyiwa upasuaji, japo hii sio mbinu inayopendelewa, ila tu ikihitajika. Pia unaweza nufaika na uchunguzi wa mtaalamu wa afya ya akili.

Mpendwa Daktari,

Ishara za ‘anorexia’ ni zipi?

Janet, Nairobi

Mpendwa Janet,

Anorexia ni neno la kimatibabu linalomaanisha kukosa hamu ya chakula. Tatizo la kususia chakula linafahamika kama anorexia nervosa, na hasa huhusisha uzani wa chini sana, mtazamo potovu kuhusu uzani na umbo, na hofu kuu ya kuongeza uzani.

Ni hali inayomsababisha mhusika kula kiwango kidogo cha chakula, na hata wakati mwingine kujilazimisha kutapika au kujihusisha na matumizi mabaya ya dawa za kufanya kinyesi kiwe chepesi ili kusababisha kuendesha.

Kwa kawaida mhusika hutawaliwa na hisia kali kuhusu mwonekano wake huku kila mara akijiangalia kwenye kioo na kujipima. Aidha, mwathiriwa atasikika kila mara akilalamika kuhusu kunenepa katika sehemu fulani za mwilii licha ya kuonekana kuwa nyembamba.

Hata, huenda akavalia nguo kadhaa ili kufunika hizi sehemu za mwili ambazo kulingana naye, zimenenepa. Dalili nyingine ni kukasirika upesi na kujitenga na wenziwe.

Kukosa kula na uzani mdogo, ni hali ambazo zaweza sababisha viwango vya chini vya damu, kisunzi, kuzimia, maumivu ya kichwa, uchovu, udhaifu, kukaukiwa, shinikizo la chini la damu, nywele kukatika, ngozi kukauka, matatizo ya kulala na mpigo usio wa kawaida wa moyo.

Hii yaweza sababisha matatizo ya moyo, figo, ubongo, mfumo wa utumbo, mabadiliko ya kihomoni, kupungua kwa mifupa na misuli na kutokuwa na msawazisho wa madini ya kieletroniki mwilini.

Matatizo haya yaweza sababisha maradhi mabaya au hata kifo, na kuna baadhi ya athari ambazo haziwezi rekebishwa.

Hali yaweza kudhibitiwa kwa ushirikiano wa daktari, mtaalamu wa lishe, mtaalamu wa kiakili, mwathiriwa, vile vile usaidizi kutoka kwa jamii (familia na marafiki).

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Wengi wakabiliwa na upofu unaoweza kuepukika

Vifo vinavyotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi...