Idadi ndogo ya wapigakura yashuhudiwa kwenye uchaguzi mdogo Juja

Na LAWRENCE ONGARO

UCHAGUZI mdogo wa kiti cha ubunge Juja umefanyika Jumanne huku idadi ndogo ya wapigajikura ikishuhudiwa.

Usalama umeimarishwa tangu asubuhi shughuli hiyo ilipoanza.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura vilionekana kuwa na wapigakura wachache huku kila mmoja aliyepiga kura akilazimika kutoka mara moja bila kupoteza wakati katika eneo hilo.

Baadhi ya vituo vya kura vilivyoonekana kuwa na wapigakura wachache ni Shule ya Msingi ya Kurahia, Gachororo, Jomo Kenyatta Primary Juja, na Magomano.

Mwaniaji wa kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee Bi Susan Njeri Waititu, amepiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Jomo Kenyatta Primary Juja, mwendo wa saa nne za asubuhi.

Alisema hata ingawa wapigakura walionekana kuwa wachache wengi wao walikuwa kwenye vibarua vyao vya kawaida lakini alitarajia kwamba majira ya adhuhuri na jioni wapigakura watajitokeza kwa wingi.

“Ninajua sasa wengi wamekwenda katika kazi zao kusaka riziki lakini kadri muda unavyosonga ndivyo wapigakura watafika vituoni kupiga kura baadaye,” alisema Bi Waititu.

Alisema ameridhika na hali ya usalama huku akitarajia uchaguzi huo utakuwa ni wa amani na haki.

Mwaniaji wa kiti hicho cha Juja kwa tiketi ya People Empowerment Party (PEP) Bw George Koimburi, alipigia kura yake katika Shule ya Msingi ya Magomano, Juja, huku akiwataka wapigakura kujitokeza kwa wingi ili wamchague kiongozi wanayemtaka.

James Mwangi wa kijiji cha Witeithie Juja alisema wanataka kiongozi atakayefanya maendeleo.

“Sisi hapa tunataka maji na barabara nzuri kwa hivyo haja yetu ni yule atakayejali maslahi ya wananchi,” alisema Bw Mwangi.

Kulingana na afisa mkuu wa IEBC wa Juja Bw Justus Mbithi shughuli ya kupiga kura ikikamilika kura zitasafirishwa hadi kituo kikuu cha kuhesabia kura kilichoko katika Shule ya Upili ya Mang’u High.