Covid: Magavana zaidi katika hatari ya kuadhibiwa

Na WANDERI KAMAU

HUENDA hatua ya Seneti kumwondoa mamlakani Gavana Mohamud Abdi wa Wajir, Jumatatu, imefungua njia kwa magavana wengine kukabiliwa kwa kutowajibikia utumiaji wa fedha za kukabili janga la virusi vya corona.

Miongoni mwa sababu zilizomfanya gavana huyo kuondolewa uongozini ni kutowajibikia matumizi ya fedha hizo, licha ya idara ya afya kutengewa Sh2.4 bilioni na madiwani.

Katika tukio la kutamausha, ilidaiwa mhudumu mmoja alifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Wajir kwa kukosa hewa ya oksijeni. Seneti ilielezwa marehemu alikuwa akiugua corona.

Kutokana na hilo, magavana wengine wako hatarini, kwani Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeonyesha kuwa zaidi ya kaunti 30 zilitumia vibaya fedha zilizotengewa serikali kukabili janga hilo.

Kulingana na ripoti hiyo, kaunti 36 zilitumia fedha hizo bila mpango maalum, utoaji mafunzo na kuzingatia utaratibu wa ununuzi wa vifaa muhimu vya kutumika kwenye juhudi hizo.

Baadhi ya kaunti hizo ni Baringo, Busia, Bungoma, Elgeyo Marakwet, Embu, Garissa, Homa Bay, Isiolo, Kirinyaga, Kisumu kati ya zingine.

Ripoti inaonyesha kaunti 23 zilitumia fedha hizo bila bajeti maalum. Kaunti hizo ni Baringo, Bomet, Bungoma, Elgeyo Marakwet, Embu, Garissa, Homa Bay, Isiolo, Kakamega, Kwale kati ya zingine.

Ripoti ilisema kuwa kijumla, kaunti zilipokea jumla ya Sh7.7 bilioni kukabili janga hilo, ambapo Sh5 bilioni zilitolewa na Serikali ya Kitaifa.

Zilipokea Sh2.3 bilioni kutoka kwa Wizara ya Afya kama marupurupu ya kuwalipa wahudumu wa afya, huku Sh350 milioni zikiwa msaada kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Denmark (DANIDA).

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Bi Nancy Gathungu, alisema serikali ilitoa fedha hizo kwa kaunti bila kuzishirikisha ifaavyo katika kubuni utaratibu maalum wa matumizi yake.

“Pengo hilo lilichelewesha matumizi ya fedha zilizotolewa. Nyingi ziliendelea kukaa kwenye benki, hali iliyohatarisha usalama wake,” akasema Bi Gathungu.

Ripoti ilionyesha kuwa kaunti zote 47 hazikuwalipa wahudumu marupurupu yao ifaavyo, nne zilitoa kandarasi kwa kampuni ambazo hazikufikisha viwango vifaavyo huku zote 47 zikikosa kufanya uchunguzi ufaao zilipotoa kandarasi kwa kampuni mbalimbali.

Hivyo, mkaguzi alisema Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) zinapaswa kufanya uchunguzi zaidi kubaini ikiwa kuna ubadhirifu mwingine uliofanyika kwenye matumizi ya fedha hizo.

“Uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa kwani kuna uwezekano kaunti nyingi zilitumia vibaya fedha zilizotengewa na serikali,” akasema.

Serikali imepokea mikopo ya zaidi ya Sh200 bilioni kukabili janga hilo tangu liliporipotiwa nchini mara ya kwanza Machi mwaka uliopita.

Hata hivyo, utata ungalipo kuhusu jinsi kiwango kikubwa cha fedha hizo zilivyotumika, hasa baada ya kuibuka kwa sakata ya Halmashauri ya Kusambaza Dawa Kenya (KEMSA), ambapo Sh7.8 bilioni zinaaminika kuporwa kupitia utoaji kandarasi ghushi.

Kaunti zimekuwa zikilaumiwa kwa kutochukua mikakati ifaayo kukabili janga hilo licha ya baadhi ya magavana kujitetea.

Habari zinazohusiana na hii

Dkt Mogusu atawagusa?