• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KINA CHA FIKRA: Pambana na hali yako ili uiboreshe, usipende kushindana na watu wengine

KINA CHA FIKRA: Pambana na hali yako ili uiboreshe, usipende kushindana na watu wengine

Na WALLAH BIN WALLAH

KATIKA safari ya maisha kila mtu ana shida zake na matatizo yake.

Watu wenye bahati huanza safari zao vizuri wakamalizia vizuri. Wapo wanaoanza vizuri wakamalizia vibaya! Na wengine huanza vibaya wakamalizia vizuri ambapo ni afadhali zaidi kuliko kuanza vizuri na kumalizia safari ya maisha vibaya!

Ajabu ni kwamba siku hizi wanadamu wameingiza hisia zao na fikra zao katika mashindano kuhusu kila kitu, kila jambo na kila kitendo. Badala ya mtu kujifanyia shughuli zake au kazi zake kwa madhumuni na malengo ya kumletea maslahi na maendeleo maishani, lazima kwanza afikirie na kuwazia ati akifanya hivi na vile atawashinda akina nani ili watambue kuwa yeye ndiye bingwa mshindi mtajika!! Lazima atafute sifa hata kama ni sifa za kashfa!!

Katika ndoto hiyo ya kuwania kuonyeshana ubabe, tabia imezuka kwamba watu wanashindana katika kutenda matendo mema na maovu!! Hapo ndipo ninapojiuliza, “Ukimshinda mtu kwa kuyatenda mema au maovu, unatarajia kutuzwa tuzo gani?” “Au siku hizi maana halisi ya kushindana yana malengo yapi ili mtu apate nini??”

Nijuavyo mimi ni kwamba mashindano muhimu humsaidia mtu kutia bidii afaulu apate mafanikio au faida ama maendeleo fulani maishani! Mashindano ni kupambana kutafuta hali bora zaidi ya kumpunguzia mtu matatizo yanayomkabili katika maisha duniani! Lakini mashindano ya siku hizi ambapo wanadamu hushindana hata kwa kutenda maovu yanayochafua maisha, ni ushindani gani? Ni mashindano yapi haya?

Kwa hakika matatizo ni mengi mno duniani! Hali ni ngumu zaidi katika maisha yetu! Badala ya kushindana kwa matendo yanayobomoa maisha kama vile chuki, ufisadi, uchoyo, wizi, majisifu, kuvaa, kula, kuua, kunyakua, matusi, kukonda, kuonea, kunenepa, kukashifiana na vituko vingine, afadhali kila mtu apambane na hali yake ngumu ya maisha ili ayatatue matatizo na shida za dunia!!

Ndugu wapenzi, juzi juzi hapa matokeo ya mitihani yalitangazwa. Shule nyingine zilipigiwa upatu kuwa zimeshinda kwa matokeo mazuri ilhali nyingine zikatajwa kwamba hazikufua dafu! Pia wanafunzi wengine walitangazwa kuwa walishinda wakawa bora zaidi ya wengine! Ushindi na ubora huo usiwe ni wa kuwakejeli wengine! Safari bado! Katika maisha kila mtu ana ubora wake!

Hakuna aliye bora kuliko watu wote duniani! Wewe mwanafunzi uliyetajwa kuwa bora, pambana na hali yako utafute pesa za kuendelea na masomo ya baadaye! Na wewe uliyenyimwa sifa za ubora, tafuta jinsi utakavyoendelea kuanzia hapo! Kila mtu apambane na hali yake badala ya kushindana na wengine!!!

You can share this post!

Wabunge kukutana kujadili na kupigia kura ripoti kuhusu...

SAUTI YA MKEREKETWA: Wanetu wafanye kozi za teknolojia ili...