• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Shughuli ya kuhesabu kura Juja yaendelea baada ya vurugu kutokea usiku

Shughuli ya kuhesabu kura Juja yaendelea baada ya vurugu kutokea usiku

Na LAWRENCE ONGARO

UCHAGUZI mdogo wa Juja ulikamilika Jumanne lakini vurumai zikishuhudiwa usiku wakati kura zilikuwa zikihesabiwa katika kituo kikuu cha matokeo kilichoko katika shule ya upili ya Mang’u High, Kaunti ya Kiambu.

Shughuli ya kuhesabu kura ilisitishwa ghafla Jumanne.

Hata hivyo mwendo wa saa mbili za asubuhi leo Jumatano, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini (IEBC) Wafula Chebukati amefika eneo la kujumuisha kura Mang’u High, na akahutubia waandishi wa habari akisema ya kwamba uchunguzi utafanywa hasa kubainisha kiini cha fuju hizo.

Uchaguzi huo umevutia wawaniaji 1, huku wakiwa na vyama tofauti.

Uchaguzi huo umekuwa na wapigaji kura wachache kabisa ikilinganishwa na mwaka wa 2017 wakati kulikuwa na asilimia 80 ya waliopiga kura.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya marehemu Francis ‘ Wakapee’ Waititu kufariki baada ya kuugua saratani ya ubongo kwa miaka miwili.

Bi Susan Njeri Waititu alihutubia waandishi wa habari majira ya saa 3 asubuhi huku akisema haridhishwi na jinsi kura hizo zinahesabiwa.

“Mimi ninataka kuona haki inatendeka kwangu. Wapigaji kura walitoa mwelekeo wao na kwa hivyo haki itendeke,” akisema Bi Waititu.

Hadi saa nne za asubuhi leo Jumatano Bw George Koimburi (PEP), amekuwa akiongoza akiwa na kura 1,644 naye Bi Susan Njeri Waititu alikuwa akimfuata kwa kuzoa kura 856. Naye Dkt Joseph Gachui amekuwa na kura 154.

Mnamo Jumanne, shughuli ya kuhesabu na kujumuisha kura ilisitishwa wakati Bw George Koimburi wa chama cha People Empowerment Party (PEP) alikuwa akiongoza akiwa na kura 858 sawa na asilimia 59 huku mpinzani wake wa karibu Bi Susan Njeri Waititu (Jubilee) akiwa na kura 439 sawa na asilimia 29. Halafu Dkt Joseph Gachui wa kujitegemea akiwa na kura 69.

Wakati huo vituo 16 pekee ndivyo vilikuwa vimewasilisha matokeo kati ya vituo 184.

Baada ya kikundi fulani kuvuruga shughuli hiyo mwendo wa saa nne za usiku walinda usalama walifurika ukumbini na shughuli ikasitishwa.

Wakati huo pia Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro na Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu Bi Gathoni Wa Muchomba walikuwa ukumbini kushuhudia kuhesabiwa kwa kura hizo.

 

You can share this post!

Manchester United wakabwa koo na Fulham katika EPL uwanjani...

Jinsi ya kuandaa milkshake ya biskuti