Raila asuta polisi kwa ukatili wao katika chaguzi ndogo

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga, ameshutumu maafisa wa polisi kwa kukubali kutumiwa vibaya na watu fulani serikalini kutekeleza vitendo vya kikatili katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Bonchari na Juja.

Kwenye taarifa Jumatano Bw Odinga amesema matumizi ya nguvu kupita kiasi na polisi katika chaguzi hizo yanawanyima wapigakura nafasi ya kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Kile kilichoshuhudiwa katika chaguzi ndogo za Bonchari na Juja ni matumizi mabaya ya mamlaka ambapo polisi walipuuza sheria na kuamua kutekeleza vitendo vibaya kabisa ambavyo msukumo wake ulitoka serikalini,” Odinga akasema kupitia Twitter.

Akaongeza: “Maafisa wa polisi wameajiriwa kuwahudumia wananchi na wala sio kuendeleza masilahi ya wale ambao wanataka kufanya majaribio ya kisiasa.”

Bw Odinga alisema kuwa maafisa walioendeleza ukatili katika chaguzi hizo ndogo wanadharau amani ambayo imedumu nchini kuanzia mwaka wa 2018.

“Watu fulani ambao wanataka kutumia handisheki kama kisingizio cha kuhujumu uhuru na amani ambayo imeshuhudiwa nchini baada ya mwaka wa 2018 wakome kufanya hivyo,” akaeleza.

Kauli ya Odinga imejiri saa chache baada ya vurugu kutokea katika kituo cha kujumuisha kura katika eneobunge la Juja, Shule ya Upili ya Mang’u. Vurugu hizo zilichangia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusitisha shughuli hiyo. Shughuli hiyo imerejelewa Jumatano asubuhi.

Na katika eneobunge la Bonchari ripoti za vyombo vya habari zilisema kuwa wafuasi wa vyama vya ODM na United Democratic Alliance (UDA) walihangaishwa na maafisa wa polisi kwa kizingizio cha kukiuka kanuni za kuzuia msambao wa corona.

Baadhi ya walioripotiwa kuhangaishwa ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Mwekahazina wa chama hicho Timothy Bosire.

Habari zinazohusiana na hii

ODM yaomboleza

ODM WAONYA UHURU