• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Sasa serikali ifufue ajenda ya chakula

TAHARIRI: Sasa serikali ifufue ajenda ya chakula

KITENGO CHA UHARIRI

KAMPUNI za kusaga unga wa mahindi zimepandisha bei tena.

Bei hiyo mpya imepanda kwa hadi Sh9 kwa mfuko wa unga wa kilo mbili.

Wanasema wamelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na uhaba wa mahindi kutoka kwa wakulima. Wengi wa wakulima hao yasemekana wameficha mahindi yao, wakitarajia kuwa uhaba wanaojitengezea utasababisha kupanda kwa bei wanayolipwa kwa juhudi zao mashambani.

Na tayari gunia la mahindi la kilo 90 sasa hivi linauzwa kwa Sh3,000 kutoka Sh2,500.

Lakini wakati wakulima wa wenye kampuni za kusaga wanapozozana, kama kawaida ya vita vya ndovu, panzi ni mwananchi. Wakenya wengi sasa hivi wanaishi kwa kudura za Mungu, kutokana na kuzongwa na matatizo ya kila aina msimu huu wa Corona.

Mbali na wafanyikazi waliopunguziwa mishahara, kuna wafanyibiashara ambao shughuli zao ziliathirika. Kampuni nyingi, kwa sababu ya kukosa wateja na mapato, ziliwafuta watu.

Kenya pia ilikumbana na janga la kiangazi katika maeneo kadhaa, mbali na wingu la nzige waliotafuna mimea na kuwapa wakati mgumu wakulima katika karibu pembe zote za nchi.

Alipoanzisha Ajenda Kuu Nne za maendeleo, Rais Uhuru Kenyatta aliweka suala la nchi kujitosheleza kwa chakula kuwa la kwanza. Masuala mengine ni Huduma za Afya kwa wote, Ustawishaji Viwanda na Makazi Nafuu.

Kupatikana kwa chakula cha kutosha kulipaswa kuanzia kwa serikali kuweka sera nzuri za kuwalinda wakulima. Kuwahimiza wapande mazao mashambani kwa kuwapa pembejeo kwa bei nafuu. Mbolea na vofaa vya kilimo vimepunguzwa bei au kuondolewa ushuru.

Serikali ilipanga kutumia Mamlaka ya Taifa ya Unyunyizaji Mashambani (National Irrigation Authority) kunyunyiza ekari 10,000 katika maeneo ya chini mwa Nzoia.

Pia kulikuwa na mradi wa kukuza mahindi wa Galana Kulalu katika kaunti ya Kilifi. Ilitarajiwa kuwa kungevunwa maelfu ya tani za mahindi.

Mipango hii mizuri yote haijafuatiliwa kikamilifu kuwezesha nchi kujitegemea kwa chakula. Muda mwingi umetumika katika siasa za majibizano na kutatiza juhudi hizo.

Kupindi hiki ambapo kampeni za Mswada wa Marekebisho ya Katiba (BBI) zimesimama, serikali ifufue ajenda yake kuhusu chakula.

You can share this post!

VITUKO: ‘Marafiki pesa’ wamwandama Pengo baada ya...

WASONGA: Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki afutwe kwa...