• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
AKILIMALI: Mwanamke aeleza biashara ya majeneza inavyompa riziki

AKILIMALI: Mwanamke aeleza biashara ya majeneza inavyompa riziki

Na WINNIE A ONYANDO

Je, wajua jinsi vitambaa vyeupe vinavyong’aa ndani ya jeneza huundwa na hata jinsi jeneza hupambwa?

Jesinter Akinyi, 29, ni kidosho na msomi kutoka mtaa wa Huruma, Kaunti ya Nairobi ni mmoja wa wale wanaotumia ushonaji sanda na kupamba majeneza kama kitega uchumi.

Kama Jesinter anavyoeleza Taifa Leo, kazi yake haijakuwa rahisi, kwani mbali na changamato za kikazi, pia kuna kasumba kutoka kwa watu kuihusiana na kazi hiyo.

“Watu wamekuwa wakiniita ‘jasanduku’ (anayehusika na majeneza) wengine wananiita ‘jamaiti’ (anayehusika na wafu) ila niliamua kuyatia nta masikioni kwa ajili ya kutafuta pesa,” Jesinter aliambia Taifa Leo.

Wengi wanaogopa hata kusikia jina jeneza likitajwa. Kinachokuja akilini ni kifo na maiti, mambo wanayochukulia kama kudra mbaya.

Kila mmoja maishani ameshawahi kumpoteza mpendwa wake katika njia moja ama nyingine. Hivyo kifo kuwa jambo la kawaida.

Kinachowapa wengi wasiwasi na uoga wa kufurahia na kuthamini kazi nzuri ya mshonaji sanda na mpambaji wa majeneza hasa huwa kumwona maiti akiwa ndani.

Kidosho huyo ambaye ni mama wa mtoto mmoja anatueleza kuwa kazi ya kushona sanda na vitambaa vya kupamba jeneza pamoja na kupamba majeneza huchukua muda na unahitaji ubunifu wa kipekee, umakini na subira ya hali ya juu.

Anaeleza kuwa alipohitimu katika Taasisi ya Ualimu Migori, ambapo alipokea mafunzo ya kuwa mwalimu wa chekechea, mwaka wa 2015, alichoshwa na kutafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio, aliamua kujiunga na shule moja ya ushonaji nguo Kariobangi, kozi aliyoifanya kwa muda wa mwaka mmoja.

Safari ya kujikimu

“Nilijaribu kushona nguo za kitenge ila zingerundika tu bila kununuliwa. Wengine wangekuambia uwashonee nguo na wakakosa kuzilipia kabisa. Ndipo nikaamua kuanzisha biashara hii na hata kuwaajiri wengine,” Jesinter aliambia Taifa Leo.

Mrembo huyo anaeleza kuwa anatumia vifaa mbalimbali katika kushona sanda na nguo za kupamba majeneza. Anaeleza kuwa kitambaa aina ya Satin ndicho hutumika katika kushona sanda na nguo ya kupamba jeneza anakinunua katika soko la Eastleigh.

Anatumia mashine ya kushona, nyuzi za rangi mbalimbali, makasi, kifaa cha kutoa uzi na kitambaa maalum nyeupe aina ya Satin. Anaeleza kuwa yeye huvishona kutokana na matakwa ya mteja.

Anaeleza kuwa kitambaa aina ya Satin hutumika katika umbapanji wa majeneza na ushonaji wa sanda kwa kuwa kinang’aa na hakichipuki ovyo. Aina hiyo ya kitambaa pia huhifadhi mwili wa maiti na hivyo kukaa kwa muda kabla ya kuoza baada ya kuzikwa.

Jesinter, mama wa mtoto mmoja anatueleza kuwa kazi ya kushona sanda na vitambaa vya kupamba jeneza pamoja na kupamba majeneza huchukua muda na unahitaji ubunifu wa kipekee, umakini na subira ya hali ya juu. PICHA/ EVANS HABIL

“Vitambaa hivyo huja katika rola na huwa ni Sh2,200 kila rola. Kila anayeuza jeneza huja kunieleza kiasi anachohitaji. Mimi huchangamkia kazi haraka,” Jesinter alieleza.

Kwa siku anawezashona vitambaa kama 10 na kila moja anaziuza kwa Sh1500. Anaeleza kuwa amejiendeleza hata kimasomo kupitia ushonaji wa vitambaa vya kubamba majeneza na sanda.

“Napenda na kuienzi kazi yangu, nalisha familia yangu, navaa, namsomesha mwanangu na hata kujiendeleza kimasomo. Sasa hivi nasoma mtandaoni namna ya kujiendeleza katika taaluma ya ushonaji usiku baada ya kufunga kazi saa kumi na mbili jioni. Sikosi soko,” Jesinter alieleza Taifa Leo.

Tangu ugonjwa wa corona kuingia nchini mnamo Desemba 2019, Jesinter anaeleza kuwa yeye hajaathiriwa sana na janga hilo kwa kuwa amekuwa akiwapata wateja kama kawaida.

“Nimeweza kuwafunza warembo wawili Everlyne na Jane kazi hii ya ushonaji, sasa hivi wanajikimu vizuri,” alisema Jesinter.

Kidosho huyo anaeleza kuwa kando na kushona nguo za kupamba majeneza, yeye huyapamba pia majeneza. Anachohitaji katika kutoa huduma zake za kupamba jeneza ni vifaa kama vile nyundo, msumari, stapla na kitambaa maalum aina ya satin alichokishona.

Kitambaaa hicho hupendelewa kwa kuwa ni laini na nyororo. Humpa maiti faraja hata anapokuwa ndani ya jeneza.

Japo jeneza hutengenezwa kwa mbao spesheli, maiti hawezilazwa katika sehemu ngumu. Ni sharti alazwe katika mahali laini na ndipo godoro laini huwekwa ndani na kando ya jeneza.

Jeneza linaweza kuundwa kutumia mti aina ya Oak, Mahogany, Elm ambayo hulainishwa na kutengenezwa katika shepu ya Chipboard ama wiani nyembamba.

Hapa seremala anahitaji vifaa kama vile mbao, nyundo, msumari, faili ya msumari, kipimo gluu ya kushika mbao, penseli, randa na handsaw (kama alivyotueleza seremala anayetengeneza majeneza David Obunga).

Seremala atavitumia vifaa hivyo katika kuunda jeneza linalohitajika. Baada ya kumaliza, kazi zinazobaki ni za mpaka rangi na mpambaji.

Mara nyingi, majeneza hupakwa rangi ya hudhurungi kwa kuwa haishiki uchafu sana na hata likishika uchafu, si rahisi kugunduliwa ikilinganishwa na rangi nyeupe.

anayepaka rangi atatumia kidude maalum aina ya bunduki na kupaka rangi ya kwanza kabla ya kupaka rangi ya kulainisha ya mwisho.

“Kwa siku, naezapamba majeneza kama kumi hivi na kila mmoja hunilipa kati ya Sh300 na Sh500 kutegemea ukubwa, upana na urefu wa jeneza lenyewe. Cha kuzingatia pia ni matakwa ya mteja,” alieleza Jesinter.

Jesinter anasema kuwa kazi yake huanzia baada ya jeneza kupitia michakato miwili muhimu hayo. Kupamba jeneza huzingatia mambo mengi sana.

Mambo ya kuzingatia katika upambaji jeneza

Cha kuzingatia kwanza ni bei ya jeneza lenyewe. Ikiwa ni jeneza linalouzwa chini ya Sh5000, anasema kuwa anatumia kitambaa nyepesi ambayo huwa ya watu ambao hawawezilipa gharama ya juu.

Jeneza la Sh10,000 kuendelea, anatumia kitambaa aina ya Satin kupamba na kuweka maridadi itakayomvutia mteja.

“Mara nyingi tunatumia kitambaa aina ya Satin, Crepe, Velvet ama Linen kulingana na mfuko wa mteja. Vitambaa hivyo huwa vya rangi nyeupe kwa kuwa watu hushirikisha uweupe na utakatifu,” Jesinter aliambia Taifa Leo.

“Hata sisi tunamtakia atakayelazwa ndani ya jeneza safari njema ndio maana tunatumia Satin nyeupe pepepe,” alitania Jesinter.

Jeneza hilo pia linawekewa bawaba, ‘mikono’, glasi ambayo sura ya maiti itaonekania na maridadi kwenye kila kona.

Baada ya hayo yote kukamilishwa, jeneza huhifadhiwa mahali ambapo halitakwaruzwa huku likisubiria mteja.

Jeneza la bei ya chini kabisa katika duka la Jesinter ni kati ya Sh5000 na 7000. Anasema kuwa kila mteja huja na matarajio yake na mifuko pia haitoshani. Jinsi anavyoeleza, katika duka lake, kuna jeneza analoliuza zaidi ya Sh100,000.

Kisura huyo anaeleza kuwa yeye hushona sanda za wamama kwa bei rahisi. Wengi hununua sanda hizo. Anaeleza kuwa mgongo wa sanda unafaa kuachwa wazi ndipo iwe rahisi kumvisha maiti.

Sanda hupambwa kutumia maridadi mbalimbali ili kuipa mvuto. Kwa siku, kidosho huyo anawezashona sanda 5 huku kila sanda ikiuza kati ya Sh3000 na Sh10000.

Katika mtaa huo huo wa Huruma Flatts, tunakutana pia na seremala mashuhuri ambaye amekuwa katika biashara ya useremala akitengeneza majeneza kwa miaka ishirini sasa.

Utengenezaji majeneza

David Obunga, 50, anasema kuwa alianza kazi ya kuunda majeneza mnamo 2001. Akisimulia Taifa Leo, Obunga anasema kuwa alijiunga na kazi hiyo pindi tu alipomaliza masomo yake ya useremala.

Obunga ambaye ana familia anaeleza kuwa alianza kupenda kazi ya useremala tangu akiwa mdogo. Baada ya kutafuta kazi kwa muda mrefu Nairobi bila mafanikio, aliamua heri kutengeneza majeneza kwa kuwa watu hufa kila kuchao.

Alikutana na mwanzilishi wa kwanza wa biashara ya kuunda majeneza katika mtaa wa Huruma Flatts Benson Muimbi ambaye alimfunza kazi hiyo kwa muda wa miezi sita. Baada ya hapo aliamua kujiajiri kupitia ujuzi na maarifa zake maalum.

“Mimi napenda kazi yangu kwa kuwa sina mvutano na mteja. Mwenye duka anapoleta vifaa vinavyotarajiwa, mimi huchangamkia kazi haraka na kutia pesa zangu mfukoni,” Obunga alieleza Taifa Leo.

David Obunga katika karakana yake mtaani Huruma, Nairobi. PICHA/ EVANS HABIL

Obunga anaeleza kuwa yeye hutengeneza majeneza mawili kwa siku na kila jeneza humpa Sh2000. Kupitia kazi yake hiyo, ameweza kuwasomesha wana wake. Mmoja yupo katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwingine akiwa katika Chuo cha kiufundi.

Kupitia kazi yake ya huku mjini, Obunga ameweza kufungua mahali pake pa kutengeneza majeneza na hata kuwaajiri vijana wengi.

Amefungua mahala pake maalum katika kaunti ya Kisumu Daraja Mbili Ceter, kando ya barabara ya Kisumu-Busia inayojulikana kama King David Services na kutoa huduma za magari ya kusafirisha mwili, majeneza, vifaa vya kuteremsha mwili na vifaa vya mazishi

Kama biashara nyingine duniani, biashara ya uundaji majeneza ina changamoto jinsi tunavyoelezwa na Obunga.

Obunga anasema kuwa wengi wamekimbilia biashara ya kuunda majeneza jambo ambalo limekuwa changamoto sana kwake.

Majeneza pia yanaweza kaa kwa muda mrefu dukani bila kununuliwa hali ambayo inafanya mapato kuwa chini.

You can share this post!

WINNIE ONYANDO: Wazazi watafute muda kuwajenga watoto wao...

Kamket ataka apewe maelezo kuhusu aliko Spika Muturi na...