• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kenya yakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo ya corona

Kenya yakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo ya corona

Na CHARLES WASONGA

KIWANGO cha maambukizi ya corona kilipanda Jumatano hadi asilimia 9.1 kutoka asilimia 7.5 Jumanne baada ya serikali kutangaza kuwa Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo.

Kenya iliandikisha visa 376 vipya vya maambukizi baada ya sampuli 4,153 kupimwa. Vile vile, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kufariki kutokana na Covid-19 ilikuwa 14 na kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 3,035.

Akiongea na wanahabari Jumanne, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuwa kuna dozi 100,000 pekee za chanjo ya AstraZeneca ilhali shughuli ya utoaji chanjo ingali inaendelea.

“Tunahitaji chanjo kwa dharura kwa sababu maghala yetu kote nchi yamesalia na dozi 100,000 za AstraZeneca. Tunahitaji chanjo kwa dharura,” akasema huku akifichua kuwa jumla ya watu 945,597 wamepokea chanjo kufikia Jumanne.

Bw Kagwe aliongeza kuwa uhaba wa chanjo ya AstraZeneca umechangiwa na ongezeko la visa vya maambukizi na maafa kutokana na corona nchini India.

Kulingana na takwimu zilizotolewa Jumatano jumla ya wagonjwa 1,074 wa corona wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini. Wagonjwa wengine 4,626 wanahudumiwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

Vile vile, wagonjwa 107 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi huku 21 miongoni mwao wakisaidiwa kupumua kwa mitambo maalum.

Wakati huo huo, jumla ya wagonjwa 318 walithibitishwa kupona corona Jumatano; 248 wakiwa ni wale waliokuwa wakihudumiwa chini ya mpango wa kuuguzwa nyumbani na 70 wakiwa na wale waliolazwa katika hospitali mbalimbali nchini.

“Kupona kwa wagonjwa 318 sasa imefikisha idadi ya waliopona kuwa 117,235,” ikasema taarifa hiyo kutoka Wizara ya Afya na kutiwa saini na Bw Kagwe.

You can share this post!

Kocha Joachim Loew arejesha wanasoka Muller na Hummels...

Balala sasa ajitetea kuhusu pendekezo la ubinafsishaji wa...