AKILIMALI: Alipoteza vyote katika ghasia za 1992 ila sasa ni mfugaji hodari wa samaki jijini

Na SAMMY WAWERU

KATIKA makazi tulivu eneo la kifahari la Kiamumbi mtaa wa Kahawa West, Nairobi, tunampata Patrick Kamau akikagua mradi wake wa kufuga samaki, anaoendesha katika kipande cha ardhi cha nusu ekari.

Anatupeleka katika kila pembe ya mradi huo wa Kiamumbi Fish Farm akitufungulia moyo kuhusu safari yake ya ufugaji wa samaki, ambayo kufikia sasa imesitiri vidimbwi 17.

“Samaki ni wanyama kipenzi changu. Ninapowapa chakula na kuona wakirukaruka na kung’ang’ania mlo dimbwini, naridhika sana,” anatanguliza.

Kamau ni mhasiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 1992 katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru. Anasema alipoteza chochote alichokuwa akimiliki kufuatia machafuko hayo mabaya.

“Vipande kadha vya ardhi, ng’ ombe na mifugo wengine na vile vile magari; hivi vikiwa tu vichache naweza kutaja,” alisema.

Kwa rehema za Mwenyeji Mungu familia yake ilinusurika lakini ikasalia salama.

Licha ya mahangaiko hayo, hakufa moyo bali alizidi kuwaza jinsi angeamka tena kusukuma gurudumu la maisha.

“Mwanamume roho ngumu! Hata ingawa makovu na hasara niliyopata yangali moyoni, nilisahau na kuwasamehe walionikosea ili nipate fursa ya kuendelea na maisha,” aliambia Akilimali katika mahojiano eneo la mradi wake.

Kamau, ambaye ana Stashahada katika Masuala ya Uhandisi, alianza upya safari ya kujiendeleza kimaisha.

Aliridhia kilimo na kuamua kujaribu ufugaji wa nguruwe. Kwa mujibu wa maelezo yake, alianza na nguruwe wanne katika mradi uliomgharimu kima cha Sh200,000.

Uliposhika kasi alifikia kuwa na nguruwe hadi 120 kwa wakati mmoja.

“Nilikuwa nikizalisha na kuuza vivinimbi (wana wa nguruwe),” aeleza.

Hata hivyo, kero ya chakula duni cha mifugo ikatibua mradi wake.

“Isitoshe, gharama ya lishe ilipanda na hatimaye sikuwa na budi kuaga ufugaji nguruwe,” anakumbuka.

Licha ya pigo hilo, Kamau hakufa moyo. Alizamia utafiti uliomwelekeza katika ufugaji wa samaki.

“Kuna programu ya ufugaji wa samaki niliyotazama kwenye runinga ikanipa motisha. Niligundua gharama ya kufuga samaki ni ya chini mno, ikizingatiwa kuwa mmoja hula gramu 0.02 ya uzito wake.”

Hali kadhalika, wanyama hawa wa majini ni nadra kuugua.

Wafanyakazi wa Kamau wavua samaki katika mradi wake wa Kiamumbi Fish Farm eneo la Kahawa West, Nairobi. CHINI: Kamau (kushoto) na msaidizi wake, Wycliffe Tete, kwenye kivungulio cha wadudu aina ya Funza Kibaha (Black Soldier Flies). Picha/ Sammy Waweru

Akiwa amejihami kwa maarifa, mwaka 2006 Kamau aliingilia ufugaji wa samaki eneo la Ruai, Kaunti ya Nairobi.

Anaambia Akilimali kwamba alianza kwa kidimbwi cha mita 15 kwa 5 mraba; ambacho kilisitiri vichengo (wana wa samaki) wapatao 500.

Alitumia mtaji wa Sh110,000 uliojumuisha malipo ya leba na gharama ya chakula.

“Baada ya miezi minane, nilivua wote; wala hakuna aliyefariki. Kila mmoja nilimuuza Sh250 (pato la jumla Sh125,000),” aelezea.

Hivyo, alivuna faida ya Sh15,000 baada ya miezi hiyo minane.

“Mapato yaliridhisha mno, nikaongeza vidimbwi viwili zaidi vikafikia vitatu huku kila kimoja kikiwa na vichengo 1, 000,” asema na kuongeza kuwa gharama hiyo ya juu haikuwa hoja kwa sababu ya hesabu ya faida aliyotazamia kutia kibindoni.

Uamuzi wa kujitosa katika ufugaji wa samaki haujutii kamwe.

Kamau, ambaye ni baba wa watoto watano, ni miongoni mwa wafugaji wanaotegemewa na masoko ya Nairobi na viunga kuzalisha samaki.

Akiwa na jumla ya vidimbwi 49 eneo la Ruai na Kiamumbi – kila kimoja kikiwa na ukubwa wa mita 17 kwa 7 mraba – huuza zaidi ya kilo 200 za samaki kwa wiki.

Kila kidimbwi kina kati ya samaki 2,000 na 3, 000.

Kamau huvua samaki walio na uzani wa gramu 400 hadi kilo mbili – kila kilo huuzwa Sh600.

Mfugaji huyu pia huongeza thamani ya samaki wake kwa kuchoma na kukaanga.

“Wateja ndio walinishinikiza kuanza kuchoma na kukaanga,” anadokeza.

Bidhaa hizo pia huzitumia katika mikahawa yake miwili eneo la Kiamumbi hapo Kahawa West na Kimbo mjini Ruiru maarufu kama Tango Gardens.

“Tunapochoma na kukaanga, tunauza Sh100 zaidi kwa kila samaki, ikiandamana na kipande cha ugali pamoja na mboga za kienyeji ambazo nakuza mwenyewe,” baba huyu asema.

Ufugaji wake ukiwa wa jijini, anasema ni ufugaji-hai. Mbali na chakula cha madukani, hujiundia chake.

Anawafuga wadudu aina ya Funza Kibaha, maarufu kama Black Soldier Flies (BSF) kwa Kimombo, ambao wataalamu wanawasifia kwa kusheheni virutubisho vya protini – madini muhimu mno kwa samaki na kuku.

“Awamu ya larvae ya BSF ina kati ya asilimia 40 – 45 ya protini-hai. Samaki wanahitaji protini kwa wingi ili kukua haraka,” anaelezea Francis Faluma, mtaalamu na afisa wa ufugaji samaki katika serikali ya Kaunti ya Kakamega.

Kulingana na Faluma, BSF ni chanzo bora cha protini ikilinganishwa na maharagwe ya soya, lishe ya dukani, mbegu za pamba na vyakula vinginevyo.

“Unavuna BSF wakiwa katika awamu ya larvae – umri wa siku 21 baada ya mayai kuanguliwa. Unachukua asilimia 20 na kuwakausha kwa miale ya jua kabla kuwapa samaki,” afafanua Wycliffe Tete, mfanyakazi wa Kamau na aliyebobea katika uzalishaji wa BSF.

Anaongeza: “Kiwango kilichosalia asilimia 20 hurejeshwa vizimbani kuendeleza uzalishaji.”

Kamau ana vivungulio (Greenhouse) viwili vya shughuli hiyo ya kuzalisha wadudu wa BSF. Wadudu hao hulishwa machicha na kinyesi cha nguruwe.

“BSF wanapotaga mayai hufariki. Mizoga yake huilisha kuku,” anadokeza mfugaji huyo na kufichua kuwa pia anafuga kuku wa kienyeji.

Baada ya kupata BSF wa kutosheleza samaki wake, wadudu wanaosalia huwauza; kilo moja ya waliokaushwa ni Sh150 huku walio hai ikiwa Sh100.

Mradi wa Kiamumbi Fish Farm pia unajishughulisha na uzalishaji vichengo, yaani wana wa samaki.

Hutumia vichengo hao katika vidimbwi vyake kuzalisha samaki wapya. Waliosalia huwauza Sh12 kila mmoja.

Wakati wa mahojiano tulimpata akiwa na zaidi ya samaki 50,000 na vichengo 150,000.

Kamau alisema kafyu iliyotolewa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona imeathiri kwa kiasi kikubwa biashara yake.

Hii ni kwa sababu ana wateja kutoka maeneo ya mbali hadi Nyanza, na ilikuwa vigumu kwake kuwafikia.

Changamoto nyingine ni kwamba wakati akianza mradi huu nusra alemewe na gharama ya chakula maalum cha samaki, kabla avumbue matumizi ya BSF.

Yeye hufuga samaki aina ya Tilapia kwa wingi pamoja na kambare (catfish). Hali kadhalika, hufuga pia samaki wa umaridadi.

Ameajiri wafanyakazi 15 katika mradi huo wa samaki.

“Ufugaji samaki unahitaji usafi wa hali ya juu katika mazingira ya vidimbwi, na hasa maji.

“Nawe mfugaji uwe mvumilivu na mwenye bidii. Kwa wanaokumbatia ufugaji huu kwa mara ya kwanza, fanya utafiti wa kutosha kuhusu samaki utakaoweka, chakula bora na soko,” adokeza jinsi ya kufanikisha ufugaji huo

Habari zinazohusiana na hii