• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Liverpool wapepeta Burnley na kuingia ndani ya mduara wa 4-bora EPL

Liverpool wapepeta Burnley na kuingia ndani ya mduara wa 4-bora EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool alifananisha ushindi wa kikosi chake dhidi ya Burnley na ufanisi wa “nusu-fainali” ambao kwa sasa umewapa tiketi ya “fainali” dhidi ya Crystal Palace katika mchuano wa mwisho kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Chini ya Klopp, Liverpool waliwapokeza Burnley kichapo cha 3-0 mnamo Jumatano usiku ugani Turf Moor na kutinga ndani ya mduara wa nne-bora kwenye msimamo wa jedwali.

Miamba hao waliotawazwa wafalme wa EPL mnamo 2019-20, waliingia ugani kuvaana na Burnley wakilenga kuendeleza ubabe uliowapa ushindi wa 2-1 dhidi ya West Bromwich Albion katika mechi ya awali mnamo Mei 16, 2021. Ushindi huo uliimarisha zaidi nafasi yao ya kuingia ndani ya orodha ya nne-bora na hivyo kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2021-22.

Wakicheza dhidi ya Burnley, Liverpool walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa fowadi Roberto Firmino mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Chipukizi Nathaniel Phillips alipachika wavuni goli la pili katika dakika ya 52 kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili. Goli la Nathaniel lilikuwa lake la kwanza ndani ya jezi za Liverpool.

Liverpool almaarufu ‘The Reds’ sasa wanakamata nafasi ya nne kwa alama 66 sawa na Leicester City wanaoshikilia nafasi ya tano kutokana na uchache wa mabao.

Masogora wa Klopp watafunga rasmi kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Palace mnamo Mei 23 mbele ya mashabiki 10,000 ugani Liverpool na mchuano huo utakuwa wa mwisho kwa kocha Roy Hodgson wa Palace kusimamia.

Kwa upande wao, Leicester almaarufu ‘The Foxes’ watakuwa wenyeji wa nambari saba Tottenham Hotspur uwanjani King Power. Chelsea ambao wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 67 wakiwaendea Aston Villa ugani Villa Park.

“Leo ilikuwa nusu-fainali ambayo tulikuwa na ulazima wa kushinda. Nafurahi kwamba tulifaulu kufanya hivyo. Kazi bado haijakamilika. Tungali na fainali ya kusakata na hilo ndilo jambo tulilolitaka,” akatanguliza Klopp.

“Tulistahili ushindi kwa sababu tuliweka wazi maazimio yetu mapema dhidi ya Burnley. Itakuwa raha tele kuwapa mashabiki wetu 10,000 kitu cha kujivunia katika gozi lijalo ugani Anfield,” akasema.

Chini ya kocha Sean Dyche, Burnley kwa sasa wana rekodi mbovu ya kupoteza jumla ya mechi 10 mfululizo za EPL katika uwanja wa nyumbani tangu Januari 2021. Kikosi hicho kitakachofunga kampeni za muhula huu dhidi ya Sheffield United ugani Bramall Lane, sasa kinashikilia nafasi ya 17 jedwalini kwa alama 39.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Juventus wapepeta Atalanta na kutwaa ubingwa wa Coppa Italia

Kigogo Sami Khedira wa Ujerumani kuangika daluga zake za...