Walinzi wa rais wamnyaka mwanamume akinyemelea jukwaani Lamu

ANTHONY KITIMO na VALENTINE OBARA

WALINZI wa Rais Uhuru Kenyatta, jana walilazimika kumzingira ghafla katika Kaunti ya Lamu ilipohofiwa maisha yake yalikuwa hatarini.

Alipokuwa akitoa hotuba yake katika uzinduzi wa sehemu ya kwanza ya kuegesha meli katika Bandari ya Lamu, kijana mmoja alisimama akionekana kuelekea jukwaani ambapo rais alikuwa akihutubu.

Kwa haraka, mlinzi wake ambaye kwa kawaida husimama nyuma ya rais alimsongelea upande wa kulia, huku walinzi wengine wengi ambao hawana sare rasmi wakitokea ghafla na kumzingira pande zote.

Baadhi ya walinzi walimchukua kijana huyo na kumwondoa ukumbini. Kufikia wakati wa kuchapisha taarifa, ilikuwa haijabainika alikuwa ni nani, nia yake, wala mahali alikopelekwa.

“Pole sana. Kila mtu na mambo yake,” akasema Rais Kenyatta baada ya tukio hilo fupi.

Baadaye akiendelea kutoa hotuba yake, alionekana kuwa mwangalifu na wakati mmoja akamwagiza mtu mwingine aliyejaribu kusimama akae chini.

Kulikuwa na ulinzi mkali ikilinganishwa na inavyokuwa katika hafla nyingine anazohudhuria kwani msafara wake ulikuwa pia na gari la polisi ambalo huwa limeekewa bunduki juu.

Viongozi wa kisiasa wa Kaunti ya Lamu walikosa nafasi ya kuhutubu katika hafla hiyo isipokuwa Gavana Fahim Twaha.

Viongozi wengine wa Lamu waliokuwepo walijumuisha Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Bi Ruweida Obbo, Seneta Anuar Loitiptip na Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama.

Mapema wiki hii, baadhi yao walikuwa wamelalamika kuwa uzinduzi huo ulikuwa umepangiwa kuendelea licha ya kuwa wenyeji bado wana malalamishi tele kuhusu mradi wa kujenga bandari.

Malalamishi yalikuwa yanahusu ajira kwa wenyeji, fidia kwa wavuvi waliopoteza sehemu zao za kazi kupisha bandari, hali duni ya usalama maeneo mbalimbali ya Lamu na ukosefu wa miundomsingi ya kutosha kustahimili mahitaji ya wafanyabiashara watakaovutiwa na bandari hiyo.

Bw Twaha alimwomba rais atenge nafasi baadaye ili wafanye mkutano kwa pamoja na viongozi wenzake kujadili masuala yaliyoibua utata.

Hata hivyo, alisifu kukamilishwa kwa gati ya kwanza na kuhimiza wakazi wajitafutie jinsi watakavyonufaika.

“Hii ni nafasi bora kwa watu kujiendeleza. Wale wanaotaka kuendelea wataendelea, na wanaotaka mizozo pia watapata. Kinachohitajika ni kila mtu atafute nafasi yake ya kujiendeleza, haitakosekana,” akasema Bw Twaha.

Katika hotuba yake, rais aliagiza wasimamizi wa Bandari ya Lamu kuwapa vijana wa eneo hilo kipaumbele katika ajira.

Jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo liliekwa na aliyekuwa rais Mwai Kibaki mnamo 2012.

Rais alikuwa ameandamana na maafisa mbalimbali wa serikali wakiwemo mawaziri Ukur Yatani (Fedha) na James Macharia (Uchukuzi).

Kuhusu usalama, Rais Kenyatta alitoa wito kwa wakazi kushirikiana na polisi akisema wahalifu ni watu wanaojulikana katika jamii.

Aliahidi serikali ya kaunti kwamba serikali kuu itasaidia kuimarisha miundomsingi ili kustahimili idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kuvutiwa na biashara ambazo zitafunguka Lamu.

Bandari hiyo inayopangiwa kuwa na gati 32 imejengwa eneo la Kilalani. Ujenzi wa gati ya pili na ya tatu unatarajiwa kukamilishwa Julai na Oktoba 2021 kwa mujibu wa Rais Kenyatta.

Meli ya Mv CAP Carmel iliyosajiliwa Singapore ilikuwa ya kwanza kuwasili mwendo wa saa kumi na moja alfajiri ikiwa imetoka Dar es Salaam, Tanzania.

Rais alishuhudia meli ya Mv Seago Bremerhavel ikitia nanga mwendo wa saa tisa mchana ikiwa imetoka Bandari ya Mombasa, na upakuaji wa mizigo kutoka kwake.

Meli hiyo ilikuwa imebeba Tani 80 za parachichi ambazo zilipakiwa kwa meli ya Mv CAP Carmel, zikipelekwa Marseille, Ufaransa.

Awali Rais Kenyatta alifungua rasmi barabara ya Garsen inayoelekea Lamu kupitia Witu, ya kilomita 114. Alizindua barabara hiyo katika eneo la Minjila lililo Garsen.

Barabara hiyo ni mojawapo ya miundomsingi muhimu ambayo itategemewa kurahisisha usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Bandari ya Lamu.

Habari zinazohusiana na hii