• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
TAHARIRI: Yafaa Rais aupime ushauri anaopewa

TAHARIRI: Yafaa Rais aupime ushauri anaopewa

KITENGO CHA UHARIRI

KUSHINDWA kwa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo uliofanywa Jumanne kunaibua maswali mengi kuhusu chama hicho tawala na washauri wa Rais Uhuru Kenyatta.

Jubilee ilishindwa kutetea viti vyote vitatu ilivyokuwa inashikilia kabla ya vifo vya wabunge wawili na MCA mmoja.

Ilipoteza Bonchari kwa ODM, Juja kwa PEP na katika wadi ya Ruire kwa UDA.

Japokuwa ilitarajiwa kuwa chama cha ODM kingekuwa na ushawishi mkubwa eneo la Nyanza, matokeo katika eneo la Mlima Kenya yaliwashangaza wengi.

Kibaya zaidi ni Jubilee kushindwa eneo la Juja, ambalo linapakana na Gatundu Kusini, nyumbani kwa Rais Kenyatta.

Mwaniaji wa chama cha PEP alishinda kwa zaidi ya kura 5,000 na kusababisha viongozi wa Jubilee wajikune vichwa wasijue kilichowapiga.

Kwa viongozi hao, huenda wakashangaa, lakini hili si jambo la ajabu. Jubilee imekuwa chama ambacho mbali na kuwa tawala, hakuna jingine linalojulikana kukihusu. Viongozi wake karibu wote walijiuzulu au kuondolewa bila ya kuwepo mkutano mkuu wa wajumbe.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti, Bw David Murathe, ameendelea kuzungumzia masuala ya chama hata baada ya kutangaza kujiuzulu. Naibu Katibu Mkuu Caleb Kositany aliondolewa kwa njia isiyoeleweka na nafasi yake ikajazwa na Joshua Kutuny.

Mabadiliko hayo ya uongozi yalifanywa kupitia matangazo ya Katibu Mkuu Raphael Tuju, bila ya wajumbe kuitwa kwenye uwanja wa Kasarani kama ilivyo kanuni ya vyama vingi vikuu vya kisiasa.

Kwamba chama cha Jubilee kiliundwa kwa pupa baada ya Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto kukubaliana wavunge TNA na URP na kualika vyama vidogo kama New Ford Kenya na kadhalika, si sababu tosha ya mgawanyiko unaoshuhudiwa.

Kutokana na Dkt Ruto kutangaza chama cha UDA na hata kusimamisha wawaniaji dhidi ya Jubilee, jambo la busara lingekuwa kuitisha wajumbe na kuidhinisha kuwa ni wakati wa mwanzo mpya.

Kuendelea kunyamaza kwa uongozi wa Jubilee kunafanya Wakenya wahisi ni kama chama hicho kilikufa zamani. Kama hali ni hiyo, basi litakuwa pigo kubwa kwa demokrasia na historia.

Rais anapaswa achukue hatamu na kuonyesha mwelekeo, hata anapoendelea kusikiza ushauri wa watu walio na malengo ya kibinafsi.

You can share this post!

Fowadi Jordan Larsson aitwa kambini mwa Uswidi kujaza pengo...

Colombia yapoteza fursa ya kuandaa fainali za Copa America...